Mapigano Burkina Faso na hofu ya COVID-19 yafurusha wakimbizi kurejea Mali
Mapigano Burkina Faso na hofu ya COVID-19 yafurusha wakimbizi kurejea Mali
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, bado lina hofu kubwa juu ya ongezekola ghasia nchini Burkina Faso, ghasia ambazo kila uchao zinafurusha watu kutoka kwenye makazi yao.
UNHCR inasema kuwa kadri ghasia zinavyosambaa kwenye ukanda wa Sahel, Burkina Faso tangu mwezi Januari mwaka huu imeshuhudia zaidi ya watu 838,000 wakisalia wakimbizi wa ndani, idadi ambayo inazidi kuongezeka kila siku huku kuwasili kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, kukiongeza chumvi kwenye kidonda cha ukosefu wa usalama.
Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumza na waandishi wa habari kutokea Geneva, Uswisi kwa njia ya video amesema kuwa mashambulizi kutoka kwa wapiganaji waliojihami pia yameathiri wakimbizi 25,000 wa Mali ambao wanaishi kwenye kambi zilizo maeneo ya ndani zaidi karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso.
Amesema ghasia zimekumba majimbo 13 ya Burkina Faso ambapo wiki iliyopita watu wapatao 32 waliuawa katika mfululizo wa mashambulizi ilhali wengine kadhaa walijeruhiwa.
"Idadi kubwa ya wakimbizi hao sasa wameamua kurejea nyumbani licha ya ukosefu wa usalama huko nyumbani kwao wakiona kuwa ni bora zaidi kuliko ukimbizini,” amesema Bwana Baloch akifafanua kuwa katika kambi ya Goudoubo ,iliyokuwa makazi ya wakimbizi 9,000, mashambulizi ya hivi karibuni yamesababisha isalie tupu kwa kuwa wakimbizi wa ndani wameamua kukimbia kusaka usalama kwingineko.
UNHCR imesema kuwa wakimbizi hao waliona kuwa kwa sababu shule zimefungwa, sambamba na kituo cha afya na kile cha usalama kwenye kambi yao, nusu ya wakazi wa kambi hiyo waliona bora wakimbie na nusu yao waliofikia maeneo ya Mopti, Gao na Timbuku walitaja ukosefu wa usalama kuwa sababu ya kurejea nyumbani kutoka Burkina Faso.
Ukurasa kuhusu virusivyacorona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.Halikadhalika wakimbizi wengine nao wamesema wanataka kurejea nyumbani Mali pindi vikwazo vitokanavyo na virusi vya Corona vitakapolegezwa.
Hata hivyo msemaji huyo wa UNCHR amefafanua kuwa pamoja na hali ilivyo sasa wanashirikiana na mamlaka kupatia wakimbizi wanaorejea nyumbani makazi, vifaa vya misaada na fedha kusaidia maisha yao sambamba na vifaa vinavyohitajika kukabiliana na janga la COVID-19.