Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Burkina Faso yawalazimisha wakimbizi wa Mali kurejea nyumbani

Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho nchini Burkina Faso(Machi 2019). Ukosefu wa usalama, mzozo wa chakula na mafuriko ni miongoni mwa vichocheo vya mzozo wa kibinadamu nchini humo.
OCHA
Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho nchini Burkina Faso(Machi 2019). Ukosefu wa usalama, mzozo wa chakula na mafuriko ni miongoni mwa vichocheo vya mzozo wa kibinadamu nchini humo.

Machafuko Burkina Faso yawalazimisha wakimbizi wa Mali kurejea nyumbani

Wahamiaji na Wakimbizi

Hali tete ya usalama inayoendelea nchini Burkina Faso inawalazimisha watu wengi kuzikimbia nyumba zao na kwenda kusaka usalama sehemu zingine au kukimbilia nchi jirani ya Mali kama wakimbizi limesema shirika la Umoja wa Msataifa la wakimbizi UNHCR hii leo.

Wakati huohuo kwa mujibu wa shirika hilo idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Mali waliokuwa nchini Burkina Faso wanasema wana hofu kubwa na wanaona ni salama kurejea nchini mwao kuliko kusalia Burkina Faso.

Katika siku 17 zilizopita UNHCR inasema jumla ya watu 14,000 wamezikimbia nyumba zao na kufanya jumla ya wakimbizi wa ndani nchinin humo kufikia 780,000.

Machafuko ya hivi karibuni pia yamewafurusha watu zaidi ya 2000 ambao wamelazimika kukimbilia nchini Mali. Kutokuwepo usalama kumefanya hali kuwa ngumu zaidi hasa kwa wakimbizi wa Mali ambao wakwenda kusaka usalama Burkina Faso na kutishia kusambaratisha juhudi za kuwasaidia kujenga upya Maisha yao.

Burkina Faso inahifadhi zaidi ya wakimbizi 25,000 kutoka Mali lakini wengi wao wamechagua kurejea nyumbani licha ya kwamba watakabiliwa na changamoto ya usalama huko pia.

Wakati huohuo UNHCR inasema inatiwa wasiwasi mkubwa na ongezeko la idadi ya watu wanaotawanywa Sahel na kutoa wito wa ulinzi kwa rai ana kwa wale wanaokimbia machafuko.