Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 700,000 watawanywa na machafuko Sahel:UNHCR

Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho nchini Burkina Faso(Machi 2019). Ukosefu wa usalama, mzozo wa chakula na mafuriko ni miongoni mwa vichocheo vya mzozo wa kibinadamu nchini humo.
OCHA
Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho nchini Burkina Faso(Machi 2019). Ukosefu wa usalama, mzozo wa chakula na mafuriko ni miongoni mwa vichocheo vya mzozo wa kibinadamu nchini humo.

Watu zaidi ya 700,000 watawanywa na machafuko Sahel:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na washirika wake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani katika eneo la Sahel huku mashambulizi dhidi ya raia yakiongezeka.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic nchini Burkina Faso mashambulizi ya karibuni yanayofanywa na wanamgambo dhidi ya raia na maafisa wa serikali yamewalazimisha watu zaidi ya 4000 kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao kila siku  kwenda kusaka usalama pengine tangu tarehe Mosi Januari.

Ameongeza kuwa “Hadi sasa watu 765,000 wametawanywa na zaidi ya laki saba miongoni mwao katika miezi 12 iliyopita. Hili ni ongezeko mara kumi zaidi ikilinganishwa na Januari 2019. Na takriban watiu 150,000 wanakadiriwa kukimbia katika wiki tatu zilizopita pekee.”

UNHCR imesema watu wanaokimbia wanaripiti kuhusu mashambulizi katika vijiji vyao kutoka kwa makundi ya wanamgambo ikiwemo “mauaji, ubakaji, na utesaji. Na kwa kuhofia mashambulizi haya wakazi wamekimbia na kuacha kila kitu kwenda kusaka usalama.”

Shirika hilo linasema zaidi ya wakimbizi 4400 kutoka Niger wamewasili Mali  wakikimbia wimbi jipya la mashambulizi katika majimbo ya Tillaberi na Tahoua, ikiwemo shambulio la mapema Januari kwenye mji wa Chinagodar.

Wakimbizi hao wamepata hifadhi katiia miji ya Andéramboukane na Ménaka nchini Mali, na watu wanaendelea kuvuka mpaka baina ya Niger na Mali kila uchao.

Nchini Mali katika majimbo ya Kati ya Segou na Niono watu Zaidi ya 1000 wamekimbilia katika nchi jirani ya Mauritania.

Likitiwa hofu na ongezeko kubwa la watu waliotawanywa sahel shirika la UNHCR limerejelea wito wake kwa pande zote katika mzozo kuwalinda raia na wale wanaokimbia machafuko.

Pia shirika hilo limesema wahudumu wa kibinadamu wanahitaji fuesa salama ya kufikia misaada ya dharura kwa maelfu ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi hususan hususan malazi, elimu, huduma kwa waathirika wa ukatili hasa wa kingono.