Mfululizo wa mashambulio umewalazimisha maelfu kuyakimbia maeneo yao Burkina Faso 

7 Mei 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR lina wasiwasi mkubwa juu ya hali ya kibinadamu nchini Burkina Faso kutokana na ghasia za siku 10 zilizopita katika mkoa wa Mashariki.  

Ghasia  zimesababisha watu 45 kuuawa na zaidi ya 17,500 kukimbia. Watu wenye silaha, kwa mujibu wa UNHCR wamefanya mashambulizi matatu tofauti ,wakichoma nyuma, kuua raia huku wakivamia na kuharibu vituo vya afya, maduka na nyumba.  

Katika Mkoa wa Mashariki zaidi ya watu 4,400 wamekimbilia miji ya Foutouri na Tankoualou kufuatia shambulio kwenye kijiji cha Kodyel. Katika Mkoa wa Kaskazini, vurugu zilisukuma watu 10,200 kukimbilia Ouahigouya eneo ambalo tayari lilikuwa limefika mapema mwaka huu. Wakati katika Mkoa wa Sahel, zaidi ya watu 3,200 wameyahama makazi yao hivi karibuni. “Timu zetu zinaona ongezeko la watu wanaokimbilia kuelekea vituo vikubwa na salama vya miji.” Imesema taarifa ya UNHCR.  

UNHCR imeeleza kuwa watu wengi wanawasili wakiwa na mali chache au hawana chochote kabisa. Wengine wamekaribishwa kwa ukarimu na familia zinazowakaribisha, wakati wengine wametafuta hifadhi katika majengo ya umma kama shule na makazi mengine ya muda. Wanahitaji chakula, malazi, maji safi, na huduma ya afya. 

“Katika Ouahigouya, timu zetu na wadau wetu, wanasajili watu wapya na kutoa msaada wa kisaikolojia na msaada wa makazi. Ukosefu wa usalama katika maeneo mengine ya Mikoa ya Mashariki na Sahel inapunguza uwezo wetu wa kufikia wale ambao wana uhitaji zaidi.” Imefafanua zaidi UNHCR. 

UNHCR inahitaji hatua za pamoja kuelekea amani na utulivu na inasimama kwa mshikamano na mamlaka ya Burkina Faso na waathiriwa wa vurugu. Pamoja na washirika wetu, tuko tayari kusaidia wale waliokimbia makazi yao na kusaidia mamlaka na kukaribisha jamii kwenye mstari wa mbele wa usaidizi. 

Kwa zaidi ya miaka miwili, vurugu nchini Burkina Faso zimelazimisha zaidi ya watu milioni 1.14 kukimbia makazi yao kutafuta usalama. Nchi hiyo inaendelea kuwa na wakimbizi zaidi ya 20,000 na waomba hifadhi, wengi wao wakiwa kutoka Mali. Rasilimali zaidi zinahitajika kushughulikia mahitaji ya kibinadamu yanayokua. UNHCR inasema ufadhili bado uko chini sana, na ni asilimia 22 tu ya dola za Marekani milioni 91.6 zilizoombwa, ndizo zimeshapokelewa hadi sasa. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter