Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waajiri saidieni familia za wafanyakazi wakati huu wa COVID-19 – ILO/UNICEF

Kazi ya kusafisha nchini Argentina
U.N. Argentina
Kazi ya kusafisha nchini Argentina

Waajiri saidieni familia za wafanyakazi wakati huu wa COVID-19 – ILO/UNICEF

Ukuaji wa Kiuchumi

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la kazi, ILO leo wametoa mapendekezo ya jinsi waajiri wanaweza kusaidia waajiriwa na familia zao wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo mjini New York, Marekani imesema kadri gonjwa hilo linavyozidi kusambaa, ni muhimu kusaidia familia kupnguza madhara yake kwa watoto wakisema kuwa, “kupoteza ajira, shule kufungwa na ukosefu wa huduma za malezi ya watto kunamaanisha kwamba familia hasa zile zenye kipato cha chini zinahitaji msaada za ziada.”

Mkuu wa masuala ya uendelezaji watoto, UNICEF, Dkt. Pia Rebello Britto amesema kuwa, “Madhara ya COVID-19 ikiwemo kupoteza ajira, msongo wa kupitiliza na kudorora kwa afya ya akili kutagusa familia nyingi katika miaka ijayo. Kwa watoto wengi walio hatarini, ukosefu wa mifumo ya kutosha ya hifadhi ya jamii kunaongeza hatari ya wao kutumbukia zaidi kwenye madhara hayo.”

Ni kwa mantiki hiyo UNICEF inasihi waajiri waangalia madhara ya uamuzi wa kazi zao kwa familia za waajiriwa na kusaidia popote pale inapowezekana.

UNICEF na ILO wanatoa wito kwa serikali kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii hususan kwa familia maskini ikiwemo kusaidia waajiriwa kuendelea na ajira na kupata kipato na kuwapatia hakikisho la usaidizi wa kifedha wale ambao wanapoteza ajira zao.

Mkurugenzi wa ILO kuhusu mazingira ya kazi Manuela Tomei anasema wao wanasisitizia mashauriano na ushirikiano baina ya serikali, wafanyakazi na waajiri pamoja na wawakilishi wa waajiriwa ikisema, “ni muhimu iwapo uamuzi wowote uweze kuwa endelevu na fanisi. Ni lazima ujengwe katika misingi a kuaminiana na kwa kuzingatia uzoefu wa aina mbalimbali.”

Mathalani, sera na vitendo ambavyo ni rafiki kwa familia kama vile ulinzi wa ajira za wafanyakazi na vipato vyao, likizo yenye malipo kwa ajili ya kuuguza au kutunza familia, saa za kazi ziendanazo na mahitaji ya mwajiriwa na kupata huduma bora ya malezi ya watoto.

Ni kwa kuzingatia msingi huo, mapendekezo ya mashirika hayo mawili ni pamoja na kufuatilia na kufuata ushauri wa mamlaka za kitaifa na kieneo na kusambaza taarifa hizo kwa wafanyakazi.

Pia kutathmni iwapo sera za sasa za pahala pa kazi zinatoa usaidizi wa kutosha kwa wafanyakazi na familia zao.

Pendekezo lingine ni kutumia mifano bora wakati wa kutekeleza sera mpya kwa kuzingatia mashauriano ya kijami, sheria za kai na viwango vya kimataifa vya kazi.

ILO na UNICEF wanataka pia waajiri wahakikishe kuwa wafanyakazi wote bila msingi wowote wa ubaguzi wan haki ya kupata msaada kazini, na kila mfanyakazi atambue msaada huo, aelewe na ajisikie vyema kuutumia.

Pendekezo lingine ni kusaidia wafanyakazi wenye watoto ili wawe na mbinu mbadala za malezi salama na sahihi ya watoto wakati huu wa janga la COVID-19.

Mapendekezo yote kwa kina yanapatikana hapa.