Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la COVID-19 latishia kusambaratisha afya na uchumi katika nchi zinazoendelea:UNDP

Masoko yafungwa nchini Uganda wakati serikali ikichukua hatua kukabiliana na kusambaa kwa COVID-19.
UN News/ John Kibego
Masoko yafungwa nchini Uganda wakati serikali ikichukua hatua kukabiliana na kusambaa kwa COVID-19.

Janga la COVID-19 latishia kusambaratisha afya na uchumi katika nchi zinazoendelea:UNDP

Afya

Taarifa iliyotolewa leo na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP imeonya kwamba kusambaa kwa virusi vya Corona, COVID-19 kunatishia kusambaratisha nchi zinazoendelea sio katika mgogoro wa kiafya pekee wa muda mfupi bali janga la kijamii na kiuchumi kwa miezi na miaka ijayo.

Shirika hilo ambalo sasa linasaka msaada kuweza kuzinusuru nchi hizo linasema hasara ya mapato kutokana na COVID-19 inatarajiwa kupita dola bilioni 220 katika nchi zinazoendelea na karibu ajira zote barani Afrika zitapotea.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya UNDP “inakadiriwa kwamba asilimia 55 ya watu wote duniani hawana fursa ya hifadhi ya jamii hasara hizi zitaathiri jamii, elimu, haki za binadamu na katika sehemu zingine uhakika wa chakula na lishe.”

Pia imeongeza kuwa hospitali zisizo na rasilimali za kutosha na mifumo duni zitalemewa nah ii inaweza kuchochewa na ongezeko la wagonjwa kwa sababu karibu asilimia 75 ya watu katika nchi zinazoendelea wanakosa fursa ya kupata sabuni na maji ambayo ni muhimu katika vita hivi.

Naye shirika la UNDP Achim Steiner ameongeza kuwa pia mazingiza mabaya ya kijamii  kama mipango mibovu ya miji na idadi kubwa kupindukia ya watu katika baadhi ya miji , huduma duni za maji taka na foleni kubwa barabarani vyote vinachangia kuathiri fursa ya vituo vya afya na hivyo kuongeza athari. “Janga hili ni mgogoro wa kiafya , lakini sio wa kiafya pekee katika sehemu kubwa ya dunia janga hili litaacha kovu kubwa sana. Bila msaada kutoka jumuiya ya kimataifa tunaharisha kugeuza mafanikio yote yaliyopatikana katika miongo miwli iliyopita na kupoteza kizazi chote kama si Maisha yao basi haki zao, fursa na utu wao.”

Kwa kushirikiana na shirika la afya duniani hivi sasa UNDP inazisaidia nchi hizo kujiandaa, kukabiliana na mlipuko huo na kujikwamua kutokana na athari zake kwa kujikita zaidi na wasiojiweza.

Tayari UNDP inasaidia mifumo ya afya katika nchi 15 ikiwemo China, Madagascar, Nigeria, Djibout na Eritrea. Na kituo maalum cha hatua za kukabiliana na COVID-19 kinaoongozwa na UNDP kimezinduliwa na kwa sasa kitatumia fedha zilizokuwepo takriban dola milioni 20 kuzisaidia nchi hizo lakini inakadiria kwamba dola milioni 500 zinahitajika kuzisaidia nchi 100 kote duniani.

Na shirika hilo limeitaka jumuiya ya kimataifa kutafakari zaidi ya athari za sasa za COVIDI-19 na kusisitiza masuala matatu katika kukabili vita hivi na kusambaa kwa COVID-19, kwanza rasilimali kuzisaidia kukomesha kusambaa kwa virusi, pili msaada wa kusaidia wakati wa mlipuko na tatu rasilimali za kuzuia kuporomoka kwa uchumi wan chi zinazoendelea.