Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njia tatu za kuisaidia Afrika kupambana na Covid-19: UNECA

Picha iliyopigwa angani ikionyesha wilaya ya Plateau mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.
UN Photo/Basile Zoma
Picha iliyopigwa angani ikionyesha wilaya ya Plateau mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.

Njia tatu za kuisaidia Afrika kupambana na Covid-19: UNECA

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya kiuchumi kwa ajili ya Afrika UNECA, imeaninisha changamoto zinazolikabili bara la afrika katika hatua Madhubuti za kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19.

Miongoni mwa changamoto hizo ni mkakati wa kujitenga na kutofanya mikusanyiko ya watu wengi lakini pia suala la kunawa mikono kila wakati ikisema ili kufanikisha hayo basi inapaswa kusitisha riba ya madeni ambayo nchi zilizoendelea zinazidai nchi hizi zisizojiweza ili kuzisaidia kupambana na COVID-19.

UNECA pia imependekeza njia tatu ambazo nchi tajiri zilizoendelea zinaweza kulisaidia bara la Afrika kupambana na janga  la virusi hivi vipya vya Corona.

Kwa mujibu wa tume ya kiuchumi kwa ajili ya Afrika ECA, “Hili ni janga la kimataifa lakini Afrika itaathirika zaidi ikibeba mzigo mkubwa na wa muda mrefu wa gharama za kiuchumi ambazo zitatishia hatua zilizopigwa, kuongeza pengo la usawa na kuzidhoofisha zaidi”

Msaada

Tume hiyo inasema nchi za Afrika zinajiandaa kwa athari mbaya zaidi za janga hili lakini zinahitaji msaada kujiandaa kwa janga la kiafya na athari za kiuchumi.

Imeongeza kuwa hatua zilizochukuliwa na Asia, Ulaya na amerika Kaskazini kama vile kujiepusha na mikusanyiko na kunawa mikono kila wakati itakuwa changamoto kwa nchi ambazo uunganishwaji wa teknolojia ya intaneti ni mdogo, zenye idadi kubwa ya watu, hazina fursa sawa za upatikanaji wa maji na fursa ndogo ya hifadhi ya jamii.

Na kwa sababu ya changamoto hizi UNECA inapendekeza njia tatu kwa mataifa 20 tajiri duniani , G-20 za kuzisaidia nchi za Afrika katika vita hivi.

 

1.Msaada wa haraka wa mahitaji ya kibinadamu

Viongozi wa G-20 ni lazima wasaidia na kuchagiza ufunguaji wa njia za biashara hususan kwa makampuni ya madawa na vifaa tiba vingine, lakini pia kusaidia kuimarisha miundombinu ya afya na kutoa msaada wa moja kwa moja kwenye vituo vilivyopo.

Kwa mujibu wa UNECA hii itaziruhusu nchi kujikita zaidi haraka iwezekanavyo na kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo na kuanza ujenzi wa vituo vya matibabu.

Msaada pia unapaswa kutolewa kwa shirika la afya duniani WHO, wakfu wa Umoja wa Mataifa, Global Fund, muungano wa chanjo duniani GAVI, na wadau wengine muhimu.

Nchi hizi zilizoendelea pia zinapaswa kusaidia kampeni ya afya ya umma na fursa za kupata taarifa .Pendekezo moja lililotolewa ni kushirikiana na sekta binafsi kuimarisha uunganishwaji wa mtandao wa intaneti kuruhusu shughuli za kiuchumi ili kuendelea na hatua za kujitenga na kusaidia kushirikiana taarifa.

2.Kuidhinishwa mara moja kwa mpango wa dharura wa kujikwamua kiuchumi

Kwa mujibu wa tume hiyo ya Umoja wa Mataifa viongozi wa G-20 wanatarajiwa kutangaza dola bilioni 100 kufadhili hatua za haraka kwa maeneo kama ya afya , hifadhi ya jamii, kuwalisha Watoto walio nje ya shule na kulinda ajira. Hadi sasa dola bilioni 50 zimeahidiwa.

 

UNECA inasema kwamba kwa kuangalia kiwango cha uchumi wan chi hizi kiwango hicho cha fedha ni saw ana matumizi yaliyoahidiwa katika kanda zingine . Fungu hilo linatarajiwa pia kujumuisha kusitisha malipo yote ya riba kwa madeni ya kitaifa yanayokadiriwa kuwa dola bilioni 44 kwa mwaka huu wa 2020. Kamisheni hiyo pia imesisitiza kwamba msaada huu utolewe kutokana na matarajio, uwazi na uwajibikaji ili mawaziri wa fedha waweze kupanga ipasavyo na asasi za kiraia zinaweza kufuatilia hilo na kuhakikisha kwamba fedha zinatumika kusaidia wale wanaozihitaji zaidi.

3.Kutekeleza hatua za dharura kulinda ajira milioni 30hasa kwenye sekta ya utalii na usafiri wa anga

UNECA inataka hatua kwa ajili ya kusaidia uingizji na usafirishaji biadaa za kilimo, sekta ya madawa na sekta ya Benki pia zinapaswa kuidhinishwa. Pia mikopo ya muda mrefu na program za kusaidia mikopo zinaweza kusaidia kuinua kipato.

Kwa mujibu wa UNECA upatikanaji wa fedha hizi ni muhimu sana ili sekta binafsi ziendelee kufanyakazi , ikiwemo biashara ndogo na za wastani ambazo zinategemea biashara ili kuendelea.

Mwisho kamisheni hiyo imesema mipango ya kitaifa na kikanda ya kufufua uchumi inapaswa kujumuisha hatua za kusaidia biashara za Afrika, kuruhusu kusitishwa kwa aina mbalimbali za malipo ikiwemo madeni.