Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa pamoja wa UN-Habitat ni msaada kwa wakazi wa mtaa wa Mathare, Kenya

Mtaa wa mabanda jijini Nairobi, Kenya, 2016.
© Julius Mwelu/ UN-Habitat
Mtaa wa mabanda jijini Nairobi, Kenya, 2016.

Mradi wa pamoja wa UN-Habitat ni msaada kwa wakazi wa mtaa wa Mathare, Kenya

Afya

Nchini Kenya hatua zaidi zimechukuliwa kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona,  COVID-19, wakati wakati huu ambapo tayari serikali imethibitisha kuwepo kwa wagonjwa 28 wa ugonjwa huo.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kufungwa kwa shule, kupunguza idadi ya wasafiri katika magari ya usafiri wa umma, kupunguza gharama ya malipo kupitia simu za mkononi na kupiga marufuku mijumuiko ikiwemo kwenye maeneo ya burudani na ibada.

Kando na hayo ushauri ambao unatolewa na wataalamu wa afya ni umuhimu wa kunawa mikono kwa angalau sekunde 20 kwa kutumia maji na sabuni. 

Hata hivyo tafiti zinaonesha kuwa kwa jamii ambazo zinaishi katika maeneo ya mitaa duni, hii inazua changamoto kwani upatikanaji wa maji safi bado ni changamoto kwa wakazi wengi hususan mijini Kenya.

Ni kwa mantiki hiyo shirika la makazi la Umoja wa Mataifa, UN-Habitat kwa kushirikiana na kituo cha mazingira cha vijana katika makazi duni huko Mathare , au Mathare Environmental One Stop Youth Centre wameungana kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi ya kunawa mikono kwa wakazi 50,000 wa kijiji cha mlango kubwa katika mtaa huo wa Mathare ulioko Nairobi, Kenya.

Lengo na mradi huo ni kulinda watu hao ambao kwa kawaida husaka maji kwenye maeneo ya umma. 

Kituo hicho kwa usirikiano na UN-Habitat ni cha kwanza cha aina hiyo kwa ajili ya kunawa mikono  ambapo mradi huo unatarajiwa kuanzishwa katika maeneo mengine ya mitaa ya mabanda ya Mathare.

Umoja wa Maitafa unasema kuwa watu wanaoishi kwenye mitaa duni wanatajwa kuwa miongoni mwa watu wanaokabiliwa na hatari ya ugonjwa wa COVID-19.

 

 

TAGS: Kenya, UN-Habitat, COVID-19, Cotonavirus, Mathare, maji