Chonde chonde wahisani tunawategemea sasa kuliko wakati mwingine wowote:UNICEF

18 Machi 2020

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF ametoa rai kwa wahisani kuendelea kunyoosha mkono hasa wakati huu dunia ikikabiliana na janga kubwa la virusi vya Corona au COVID-19.

Henrietta Fore katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi amesema sasa kuliko wakati mwingine wowote tunawategemea wahisani wetu kuendelea kusaidia kazi zetu kwa ajili ya kuwafikia wale wasio na chochote au yeyote licha ya kwamba huu ni wakati mgumu.”

Ameongeza kuwa ikiwa ni wiki moja tangu virusi vya Corona kutangazwa kuwa zahma ya kimataifa idadi ya visa inaendelea kuongezeka kote duniani. Pia amesema “mamilioni ya Watoto hawahudhurii shule, wazazi na watoa huduma wote wanafanyia kazi waliko inapowezekana, mipaka inafungwa na maisha yamepinduliwa. Na haya ni maji marefu kwetu sote”.

Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019)
© UNICEF/Frank Dejo
Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019)

Ameongeza kuwa kwa upande wa UNICEf wanakabiliana na virusi hivi vipya vya corona, mila potofu na taarifa zisizo sahihi huku wakihakikisha usalama na afya njema kwa wamafanyazi wa shirika hilo na familia zao.

Amesisitiza kwamba “kazi yetu ya kuokoa maisha kwa kuwapa watoto afya njema, elimu, lishe na ulinzi sasa ni muhimu sana.”

Amesema wakati mamilioni wametawanywa, kuathirika na vita, kufa kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika, kukosa masomo au kukosa chanjo muhomu, haja ya msaada ni kubwa sana.

Hivi sasa amesema UNICEF inafanya kila kila iwezalo kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi miongoni mwa jamii katika nchi zilizoathirika. “tunatoa taarifa sahihi kuhusu jinsi gani ya kuhkikisha familia ziko salama, kuwapa vifaa vya usafi na kujisafi mashuleni, vituo vya afya na kudhibiti athari za mlipuko kwa fursa ya watoto kupata huduma za afya, elimu na huduma za kijamii.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter