Tukisalia nyumbani kujikinga na COVID-19, tusiwasahau wasio na makazi:UN

18 Machi 2020

Wakati huu ambapo serikali zikitegemea watu kusalia nyumbani ili kusaidia kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Corona, COVID-19, ni lazima nchi zichukue hatua za kuzuia mtu yeyote kukosa makazi na kuhakikisha fursa ya mahali pa kukaa kwa wale wasio na makazi.

Wito huo umetolewa leo na mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi bora Leilani Farha ambaye ameongeza kuwa “Makazi yamekuwa ni silaha ya msitari wa mbele katika vita dhidi ya virusi vya Corona. Nyumba hivi sasa imekuwa ni muhimili baina ya hali ya maisha au kifo. “

Ameongeza kuwa kuna mambo yanayompa wasiwasi mkubwa “Nina hofu kubwa kuhusu makundi mawili ya watu, wale wanaoishi katika makazi ya dharura, wasio na makazi na makazi yasiyo rasmi, na pili wale ambao wanakabiliwa na kupoteza ajira na hali mbaya ya kiuchumi hali ambayo itasababisha changamoto ya kulipa mikopo ya nyumba, kodi ya pango na kukabiliwa na kufukuzwa katika makazi yao.”

 

Kwa mujibu wa mtaalam huyo takriban watu bilioni 1.8 duniani kote wanaishi bila makazi na kwenye makazi duni, na mara nyingi katika hali ya msongamano, wakikosa huduma za msingi kama maji na usafi na hivyo kuwafanya kuwa katika hatari ya kukabiliwa na virusi hivi vipya hasa kwa kuwa mara nyingi wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiafya.

“Nitazitaka nchi kuchukua hatua zaidi kuhakikisha haki ya makazi kwa wote ili kuwalinda na zahma hii ya Corona.Kuna baadhi ya nchi wanachukua hatua nzuri ikiwemo kusitisha kuwafurusha watu wasiolipa kodi ya pango au kuchelewa kulipia mikopo ya nyumba hasa kule walikoathirika na virusi vya Corona, ambako majira ya baridi kali bado yanaendelea na kwa wale wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi. Pia kuna wale wanaotoa huduma kama za maji safi na usafi kwa wasio na makazi tunaomba hili liendelee kwa wote.” Amesema mtaalam huyo.

Pia ameongeza kuwa wakati hatua muhimu zinahitajika kukabiliana na hatari ya makundi haya ya watu  na kushughulikia kiwango cha maambukizi mtaalam huyo maalum amesema ili kuhakikisha ulinzi kwa wasio na makazi au wanaoishi katika makazi duni “nchi lazima zisitshe kesi zote za kuwafurushwa makwao watu , ziwape makazi ya mud ana huduma za msingi wale waliathirika na virusi vya Corona na kuwatenga, kuhakikisha hatua za kudhibiti kama watu kutotembea hovyo hazisababishi adhabu kwa yeyote kutokana na hali ya makazi yake. Pia nchi zitoe fursa sawa ya upimaji na huduma za afya na pia kutoa nyumba kama inahitajika wakati wah aliya tahadhari na dharura ikiwemo kutumia nyumba zilizo wazi au kutelekezwa kwa ajili ya muda mfupi.”

Kwa wanaokabiliwa na kukosa ajira

Na kwa wale wanaokabiliwa na kupoteza ajira na kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na mlipuko huu wa Corona mtaalm huyo ana wito “ Nchi ni lazima zitoe msaada wa fedha kwa ajili ya kodi ya pangoo au kulipia mikopo ya nyumba, zisitishe hatua ya kuwafukuza watu kwa sababu ya malipo, zianzishe njia ya kupunguza kodi ya pango japo kwa wakati wa mlipuko na pia kusitisha kwa muda gharama za malipo ya matumizi mengine kama maji, umeme na gesi.

Amesema hadi sasa “Kuna hatua zimeshachukuliwa na fungu la fedha kutengwa ili kukabiliana na athari za kiuchumi zitakazosababishwa na Corona ikiwemo mdororo wa kiuchumi kama vile kupunguza kiwango cha riba. Hata hivyo amesema kuna hatari ya hatua hizo kutumika vibaya na kuitumia fursa za janga hili kutawala soko la nyumba bila kujali viwango vya haki za binadamu  kama ilivyofanyika wakati wa mdororo wa kiuchumi wa kimataifa mwaka 2008. Hivyo nchi lazima zizuie hulka hiyo ya taasisi na wawekezaji katika upande wa nyumba za makazi.

Amesisitiza kuwa “Kwa kuhakikisha fursa ya nyumba bora na usafi sio tun chi zitawalinda watu wake na kuokoa maisha ya wasio na makazi , bali pia zitasaidia kuilinda dunia dhidi ya COVID-19.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter