Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani wa UN kutoka Burundi auawa CAR, Guterres azungumza

Kofia ya chuma  ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa
UN /Marie Frechon
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa

Mlinda amani wa UN kutoka Burundi auawa CAR, Guterres azungumza

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umeripoti hii leo ya kwamba mlinda amani wake kutoka Burundi ameuwa kwenye mji wa Grimari ulioko katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaeleza waandishi wa habari jijini New York Marekani ya kwamba mlinda amani huyo alikuwa anahudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA.
“Kisa hicho kimetokea wakati walinda amani walipokuwa wanajaribu kukabili shambulio kutoka wanamgambo waliojihami wa kundi la anti-Balaka,” amesema Dujarric.

Kufuatia tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa taarifa kupitia msemaji wake akieleza masikitiko yake makubwa huku akituma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na serikali ya Burundi.

Wakati huo huo Katibu Mkuu amelaani vikali shambulio lingine lililofanywa siku hiyo hiyo ya Jumapili na vkundi vha RPRC na PRNC dhidi ya walinda amani wa MINUSCA waliokuwa doria ambako mlinda amani mmoja kutoka Pakistani alijeruhiwa.

Shambulio hilo limefanyika katika eneo la Ndélé -Birao mkoa wa Bamingui-Bangoran, ambapo Katibu Mkuu amemtakia ahueni ya haraka mlinda amani huyo.
 
Bwana Guterres amekumbusha kuwa mashambulio yanayolenga walinda amani yanaweza kuwa halifu wa kivita kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

Ametoa wito kwa serikali ya CAR kufanya jitihada zote kubaini watekelezaji wa mashambulio hayo mawili na ili wafikishwe mbele ya sheria.
 
Katibu Mkuu amesisitiza azma ya MINUSCA ya kuendelea kutekeleza majukumu yake hususan yale ya kulinda raia na kusaidia kusongesha mchakato wa amani nchini humo.

Mapema Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkuu wa MINUSCA,  Mankeur Ndiaye, naye ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mlinda amani huyo pamoja na serikali ya Burundi.
Ameongeza kuwa walinda amani tayari wameimarisha doria kwenye eneo hilo ili kuakikisha ulinzi wa raia na pia kuepusha shambulizi lingine.