Licha ya changamoto CAR, misingi ya amani ya kudumu imewekwa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na kikao kuhusu Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambapo wajumbe wamepokea ripoti ya Katibu Mkuu wa umoja huo kuhusu utendaji wa ujumbe wa chombo hicho nchini humo, MINUSCA.
Akihutubia wajumbe kwa njia video kutoka Bangui, mji mkuu wa CAR, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini humo na mkuu wa MINUSCA Parfait Onanga-Anyanga, amesema licha ya changamoto zinazoendelea kuikumba nchi hiyo, nchi hiyo imeweka misingi ya amani ya kudumu.
Bwana Onanga-Anyanga amesema “mwelekeo wa amani na maridhiano hautakuwa rahisi na kwamba jamii ya kimataifa ni lazima ishirikiane na serikali ya CAR kuhakikisha kuwa mchakato wa amani unakuwa jumuishi na haukwami.
Amesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira yatakayopatia fursa ya kufanikiwa mfumo wa Afrika wa kuleta amani akimaanisha kuwa “hii inamaanisha kuwa pande zote husika zishiriki kwenye mazungumzo kwa nia ya dhati na nia njema ili mazungumzo yawe na mafanikio.”
Halikadhalika Bwana Onanga-Anyanga amesema ni vyema kuwa Baraza la Usalama liwe na msimamo mmoja kuhusu mchakato wa amani CAR sambamba na nchi jirani na jamii ya kimataifa kwa ujumla.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Koen Vervaeke, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya masuala ya Afrika kwenye Muungano wa Ulaya amesema ni muhimu kwa pande zote kinzani CAR zikajikita katika mchakato wa amani na maridhiano na kwamba, “suluhu ya mzozo unaoendelea ni kupitia nchi za mazungumzo na si kijeshi.”
Bwana Vervaeke ameongeza kuwa Muungano wa Ulaya kwa upande wake umeazimia kuendeleza ushiriki wake wa dhati kusaidia CAR.
Mzozo kati ya waumini wa kikristho na kiislamu ulianza huko CAR mwaka 2013 na baada ya kupungua kidogo mwaka 2015 ulirejea tena mwaka 2016 na kusababisha ghasia kuenea nchini humo.
MINUSCA ilipelekwa nchini humo mwaka 2014 ikiwa na mamlaka ya kulinda raia, kusaidia kipindi cha mpito cha kisiasa na usambazaji wa misaada ya kibinadamu sambamba na upokonyaji wa silaha na kujumuisha wapiganaji kwenye jamii.