Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaendelea kuchukua hatua zaidi dhidi ya COVID-19

Wengi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wameondoka kwenye jengo la UN na wanafanyia kazi nyumbani.
UN Photo/Loey Felipe
Wengi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wameondoka kwenye jengo la UN na wanafanyia kazi nyumbani.

UN yaendelea kuchukua hatua zaidi dhidi ya COVID-19

Afya

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani hatua zinaendelea kuchukuliwa kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 unaoitikisa dunia hivi sasa.

Tayari Umoja huo umefunga milango yake kwa ziara za umma na wafanyakazi kwa asilimia kubwa wanafanyia kazi nyumbani.

Lakini kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric kwa waandishi wa habaro sasa kuanzia tarehe 16 Machi hadi mwisho wa mwezi Aprili vikao vingi vya kando vilivyokuwa vifanyike kwenye makao makuu sasa vimesitishwa. “Katibu Mkuu António Guterres amewajulisha nchi wanachama na maafisa mbalimbali kwamba mikutano yote ya kando kuanzia Machi 16 hadi mwisho wa Aprili kwenye makao makuu mjini New York imefutwa.”

Na kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Baraza la haki za binadamu limesitisha kikao chake kuanzia leo na mikutano mingi mengine kupunguzwa.

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Vienna Austria imearifu kwamba wafanyakazi watafanyia kazi nje ya jingo la Umoja wa Mataifa kwa siku 30.

Umoja wa Mataifa pia umetangaza hatua mpya za kusaidia kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo vipya vya Corona na kupunguza hatari ya maambukizi katika majengo na ofisi zake sehemu mbalimbali duniani.

Lengo kubwa

Umoja wa Mataifa unasema lengo kubwa la kuchukua hatua zote hizo ni kujaribu kudhibiti athari za COVID-19 kwa kupunguza safari na kukutana na watu wengi. Jumatano wiki hii shirika la afya duniani WHO lilitangaza kwamba COVID-19 sasa ni zahma ya kimataifa kutokana na kusambaa kwake katika mataifa mengi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tayari ametoa wito wa kuwepo uwiano baina ya maafisa wa usalama na wawakilishi wa nchi na haja ya kuhakikisha kwamba kazi za shirika zinaendelea mjini New York na kwingineko duniani huku usalama na afya za watu zikiwa ndio kipaumbele.

Hatua zingine zinazochukuliwa

Makao makuu ya Umoja wa Mataifa hatua ya pili nay a tatu ya kukabiliana, kudhibiti na kuratibu dharura za kiafya. Hatua hizo ni pamoja na kufanyia kazi nyumbani na kupima hatari ambayo inaweza kuhusiana na safari au mikutano.

Ziara za kuzuru makao makuu ya Umoja wa Mataifa zinazofanywa na umma kila siku zimesitishwa na usafi mkubwa unazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kemikali za kuuwa vijidudu kwa kusafisha mikono.

Kisa cha kwanza kinachohusiana na makao makuu ya Umoja wa Mataifa kimetangazwa jana alhamisi kikiwa ni cha mfanyakazi kutoka nchi mwanachama anayefanya kazi na ubalozi wa kudumu wa Ufilipino kwenye Umoja wa Mataifa.