COVID-19: Idadi ya wanaoingia jengo la UN New York yapunguzwa kwa asilimia 60 wakiwemo wafanyakazi

11 Machi 2020

Wakati maambukizi mapya ya virusi vya Corona au COVID-19 yakiendelea kuongezeka katika nchi nyingi duniani na idadi ya waliofariki kutokana na virusi hivyo ikiongezeka kila uchao, Umoja wa Mataifa nao umechukua hatua kudhibiti maambukizi kwa kupunguza idadi ya wafanyakazi wanaofika kazini kila siku kwa asilimia 60. Hii ni kwa kuzingatia kuwa tayari visa vimeripotiwa katika miji kadhaa ikiwemo New York, Marekani ambako ndiko makao makuu ya chombo hicho.

Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO hadi sasa wagonjwa waliothibitishwa kuwa na virusi vya Corona ni takribani 113,900 huku vifo ni zaidi ya 4000 na takwimu hizo ni kutoka nchi 110 zikiwemo China na Marekani.
Ni kwa kuzingatia kuendelea kusambaa kwa virusi hivyo ikiwemo hapa Marekani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema,“Virusi vipya vya corona vinatoa changamoto kwetu sote.Tunahitaji kuwa tayari na kukabiliana na changamoto hii, kwa pamoja. Ninatowaombeni nyote: Kuwa salama- kwa kufuata ushauri wa kitabibu, kisayansi na kuchukua hatua za msingi kwa mfano kunawa mkono vizuri na mapendekezo mengine ya mamlaka za afya. Pata taarifa na fuatilia ushauri kutoka kwa serikali na shirika la afya ulimwenguni. Wajali wengine na kuhakikisha kwamba hamna mtu anakabiliwa na unyanyapaa. Na kwa pamoja, hebu tuwe wajanja na kupigana na COVID-19 kwa pamoja kama Umoja wa Matafa.

Tahadhari hiyo imeelekezwa hata kwa wafanyakazi wa Umoja huo ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya mawasiliano kimataifa  Melissa Fleming

wafanyakazi wanatakiwa kufanyia kazi nyumbani kuanzia Machi 10 hadi Machi 31 kwa siku tatu kila wiki hii .

Nasi pia kwenye Idhaa ya Kiswahili sambamba na idhaa nyingine 8 za Umoja wa Mataifa, tumefuata agizo hilo na kwa hiyo tunafanya kazi kwa kupishana wengine ofisini na wengine kutoka nyumbani.

Hatua nyingine ni kwamba kuanzia jana Machi 10, jengo la Umoja wa Mataifa limefungwa kwa umma hadi itakapotangazwa tena na hiyo ina maana kwamba safari za kutalii jengo la Umoja wa Mataifa zimesitishwa kwa muda.

Kwa sasa Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia hali kwa karibu kwa ajili ya kutoa ushauri muafaka kuendena na hali hii ambayo inabadilika kila uchao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter