Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Corona isituchanganye, tuchukue hatua; Syria nako ni janga linalotia shaka zaidi- Guterres

Kituo cha udhibiti wa magonjwa, CDC, nchini  Marekani kimeanza operesheni zake za dharura kusaidia wadau wa afya katika kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona duniani.
CDC/James Gathany
Kituo cha udhibiti wa magonjwa, CDC, nchini Marekani kimeanza operesheni zake za dharura kusaidia wadau wa afya katika kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona duniani.

Corona isituchanganye, tuchukue hatua; Syria nako ni janga linalotia shaka zaidi- Guterres

Afya

Makombora yakizidi kumiminikia raia wasio na hatia nchini Syria, huku virusi vya Corona navyo vikizidi kusambaa maeneo mbalimbali duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari na kuhusu zahma hizo akisema  kuwa kwa Corona huu si wakati wa kuchanganyikiwa na kwa Syria, janga hilo ni moja ya mazingira ya kutia shaka zaidi kwenye muongo wa sasa.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Guterres amesema, “hii leo, shirika la afya ulimwenguni limeongeza tathmini yake ya hatari ya ugonjwa huo duniani, kuwa ni ya juu sana. Huu si wakati wa kuogofya, ni wakati wa kujiandaa, kujiandaa kikamilifu. Huu ni wakati kwa serikali zote kuimarisha na kufanya kila liwezalo kudhibiti huu ugonjwa na kufanya hivyo bila unyanyapaa na kwa kuheshimu haki za binadamu.”

Katibu Mkuu amesema kuwa “tunafahamu ya kwamba udhibiti unawezekana, lakini fursa nayo ya kufanya hivyo inapungua.”

Kwa mujibu wa WHO, katika saa 24 zilizopita, China imekuwa na idadi ndogo zaidi ya wagonjwa wapya kwa zaidi ya mwezi mmoja ambayo ni 329, na hivyo visa kwa  ujumla kuwa ni wagonjwa 78,959.

Halikadhalika zaidi ya watu 36,000 nchini humo wamepona ugonjwa huo usababishwao na virusi hivyo ya Corona.

Kwingineko duniani, hata hivyo, kumekuwepo na ongezeko la maambukizi mapya ambapo hadi sasa kuna visa 4351 katika mataifa 49 na kati yao hao wagonjwa, 67 wamefariki dunia.

Nchini China wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona, watu kwenye foleni ya chakula, wanasimama mbalimbali kwa hofu ya maambukizi.
Man Yi
Nchini China wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona, watu kwenye foleni ya chakula, wanasimama mbalimbali kwa hofu ya maambukizi.

Zaidi ya chanjo 20 dhidi ya virusi vya Corona zinaandaliwa- WHO

Mapema akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa wagonjwa 24 wa COVID-19 wametoka Italia na kwenda katika mataifa 14 ilhali wagonjwa 97 kutoka Iran wamekwenda katika mataifa 11.

“Ongezeko la idadi ya wagonjwa sambamba na  nchi zilizoathirika katika siku za karibuni bila shaka ni jambo linalotia hofu,” amesema Dkt. Tedros akiongeza kuwa wafuatiliaji wa magonjwa wa WHO wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hali ya sasa na wameongeza kiwango cha hatari ya ugonjwa huo duniani na kufikia kiwango cha juu kabisa.

Amesema kutokana na tangazo hilo la kiwango cha juu cha hatari, serikali zinapaswa kuelimisha umma, kupanua wigo wa ufuatiliaji, kusaka, na kutenga na kuhudumia kila mgonjwa na kufuatilia watu waliokuwa karibu na mgonjwa na kuwa na kuzingatia mfumo wa kiserikali na kijamii katika operesheni .

Amesema kuwa nchini Nigeria, mgonjwa wa kwanza amethibitishwa kuwa na virusi vya Corona na ameshatengwa.

“WHO ina imani kubwa na Nigeria katika kudhibiti virusi hivyo kutokana na ukweli kwamba taifa hilo lilifanikiwa katika kushughulikia milipuko mingine kama vile homa ya Lassa na Surua,” amesema Dkt. Tedros.

Kwa sasa tayari zaidi ya aina 20 ya chanjo dhidi ya COVID-19 zinatengenezwa maeneo mbalimbali duniani, sambamba na dawa za tiba, na matokeo yanatarajiwa kutangazwa wiki chache zijazo.

Mzozo wa Syria ukiingia mwaka 10, hali bado ni tete

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii jijini New  York Marekani kuhusu kile kinachoendelea Syria
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii jijini New York Marekani kuhusu kile kinachoendelea Syria

Kuhusu Syria, Katibu Mkuu amerejelea wito wake ambao amekuwa akitoa hivi karibuni kuwa chuki huko kaskazini-mashariki ya Syria zinaweza kuchochea madhara zaidi katika mzozo huo wa Syria unaokaribia kuingia mwaka wa 10.

“Nina hofu kubwa kwa matukio  ya saa 24 zilizopita, tunafikia hali hiyo. Hali ya sasa ni moja ya mazingira yanayotia hofu zaidi katika mzozo wa Syria. Hata maeneo ya kambi na kwingineko ambako familia za wakimbizi zinasaka hifadhi nayo pia yanashambuliwa kwa makombora,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu amesema  jambo muhimu hivi sasa ni sitisho mara moja la mapigaon kabla hali haijazidi kuwa mbaya na kushindwa kudhibitiwa.

“Katika mawasiliano yangu yote na pande zote husika, nimekuwa na ujumbe mmoja tu: Achana na hatua zitakazoleta mapigano zaidi,” amesema Bwana Guterres.

Akitambua kuwa mzozo huo unaingia mwaka wa 10 tangu uanze, Katibu Mkuu amesema kuwa muongo mmoja wa mapigano haujaleta chochote kile zaidi ya uharibifu na machungu.

“Hakuna suluhu ya kijeshi. Njia pekee ni mchakato wa kisiasa unaowezeshwa na Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa azimio namba 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Namkumbusha kila mmoja kuwa azimio hilo linataka sitisho la mapigano nchini kote,” ametamatisha Katibu Mkuu.