Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapishi ya mkimbizi kutoka Syria yabisha hodi kwa Angela Merkel Ujerumani

Kutoka maktaba: Mlo wa familia Chon Kremin Valley 10 Septemba mwaka 2019
UNICEF/Bektur Zhanibekov
Kutoka maktaba: Mlo wa familia Chon Kremin Valley 10 Septemba mwaka 2019

Mapishi ya mkimbizi kutoka Syria yabisha hodi kwa Angela Merkel Ujerumani

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Ujerumani, mwanamke mmoja mkimbizi kutoka Syria ametumia stadi zake za mapishi ya vyakula vya kwao na kujikuta anafungua mgahawa unaotoa huduma kwa watu mashuhuru akiwemo Kansela wa nchi hiyo ya Ulaya Angela Merkel. 

Mkimbizi huyo Salma Al Armarchi ni mpenzi wa mapishi lakini hali ya kupika tu kujifurahisha ilifikia ukomo mwaka 2016 alipoombwa apike chakula kwa ajili ya kulisha wafanyakazi wa kujitolea kwenye shule moja iliyoko mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, shule ambayo mwanae mkubwa Fadi alikuwa anapata mafunzo.

Salma ambaye alikimbilia Ujerumani na wanae wawili mwaka 2012 na kuungana na Fadi mwaka 2014 alikuwa salama lakini maisha  yalikuwa magumu.

Kujifunga lugha ya Kijerumani, ilikuwa jambo gumu na hivyo ikawa vigumu kupata ajira.

Hata hivyo ujio wa makumi ya maelfu ya wakimbizi wa Syria mjini Berlin mwaka 2015, ulifungua njia ambapo katika kuwasaidia na kuwapatia chakula, bahati yake ikafunguka.

“Ninapopika, najisikia furaha kwa sababu nakumbuka wakati napika na wenzangu huko Syria. Na sasa ninafurahia sana kupika na familia yangu jikoni. Kwa kweli hupika kwa upendo na furaha.”

Sifa ya mapishi  ya Salma ilienea na idadi ya wateja ikaongezeka hadi akafungua jiko lake akilipatia jina Jiko la Yasmini kwa kuzingatia kuwa anatumia viambato vya Ujerumani kupika mapishi  ya Syria.

Salma alijumuisha wanae akiwemo Fadi kuwa wafanyakazi kwenye jiko hilo  ambapo Fadi anasema,

“Tuna aina mbalimbali za vyakula ambavyo watu hawajawahi kuvila. Na vina afya, na mara nyingi tunajikita zaidi katika ubora na si wingi. Vyakula vya kupika wenyewe. Kwa hiyo tunahakikisha kila kitu ni kipya na bora  na bila shaka mama yangu ana mapishi mazuri.”

Wateja wao ni pamoja na Facebook, McKinsey, ofisi za balozi n ahata ofisi ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel na ndoto yao ni kuboresha huduma zao ili wapate wateja wengi zaidi.