Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita vikiisha Syria, nitarejea na kufungua duka la mikate ya kijerumani- Mkimbizi

Mohamad Hamza Aleman (kushoto) mkimbizi kutoka Syria akipokea mafunzo ya uokaji mikate kutoka kwa  Björn Wiese nchini Ujerumani.
UNHCR/Gordon Welters
Mohamad Hamza Aleman (kushoto) mkimbizi kutoka Syria akipokea mafunzo ya uokaji mikate kutoka kwa Björn Wiese nchini Ujerumani.

Vita vikiisha Syria, nitarejea na kufungua duka la mikate ya kijerumani- Mkimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Ujerumani, mmiliki mmoja wa duka la kuoka mikate ameleta matumaini kwa vijana wakimbizi ambao awali walihisi maisha yao yametumbukia nyongo kutokana na changamoto walizokuwa wanakumbana nazo ikiwemo lugha na fursa za kujiendeleza. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Ndani ya duka la kuoka mikate la Privatbäckerei Wiese mjini Eberswalde, kaskazini -mashariki mwa Ujerumani, anaonekana Mohamad Hamza Aleman akiwa bega kwa bega na mmliki wa duka hili Björn Wiese. Wiese anaelezea sababu ya hatua hii.

“Tuna uhaba mkubwa wa watu wenye stadi, hivyo inakuwa vigumu kupata wanaotaka kujifunza uanagenzi. Hivyo tumefungua milango kwa wakimbizi lakini pia tunataka kuwapatia stadi na fursa vijana. Hii ni kama gundi inayoweka pamoja jamii yetu:tunaposhikamana na kuwapatia watu fursa.”

Mohamad mkimbzi kutoka Syria mwenye umri wa miaka 23 aliwasili Ujerumani mwaka 2015 na anasema hakutaka kusalia nyumbani bila kufanya chochote na alipopata fursa ya kujifunza kuoka mikate hakusita.

Baada ya kumudu kuoka mikate, Mohamed aliomba ajifunze stadi za mauzo ambapo itamchukua miaka mitatu wakati huu ambapo tayari ni muajiriwa wa kudumu, ombi ambalo alikubaliwa na muajiri wake.

“Kazi yangu ina maana kubwa kwangu: Kukutana na wateja, kuzungumza nao kwa kijerumani na pia fursa ya kupata cheti nikihitimu uanagenzi na kuwa na maisha bora baadaye.”

Lengo la Mohamad ni kwamba vita vitakapokoma nchini Syria atarejea nyumbani na kupeleka utamaduni wa Ujerumani kwa njia mbalimbali ikiwemo kufungua duka la kuoka mikate ya kijerumani.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema kuwa fikra chanya za wamiliki wa biashara kama Björn Wiese sambamba na mameya wa miji na hamii zinasaidia kuleta utengamano kwenye maeneo mbalimbali nchini Ujerumani.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Ujerumani, Dominik Bartsch anasema “hawa ndio kichocheo, hawapotezi muda kufikiria siasa za ujumuishi bali wanasonga mbele, wanazungumza na wakimbizi kama binadamu walio sawa na kuleta matumaini yaliyo dhahiri.”

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.