Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake 10 watengeneza filamu toka Afrika kupata mafunzo kwa msaada wa UNESCO

UN News ilizungumza na Thamyra Thamara, mmoja wa wakurugenzi wa filamu hiyo.
Valda Nogueira
UN News ilizungumza na Thamyra Thamara, mmoja wa wakurugenzi wa filamu hiyo.

Wanawake 10 watengeneza filamu toka Afrika kupata mafunzo kwa msaada wa UNESCO

Wanawake

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO Audrey Azoulay na mtayarishashi filamu mashuhuri kutoka Japan NaomiKawase leo Alhamisi wametangaza majina 10 ya washindi wa tuzo ya UNESCO kwa ajili ya watayarishaji vijana wa filamu ambao ni wanawake toka barani afrika ilijulikanayo kama Nara Residency for Young African Female Filmmakers.

Tangazo hilo limetolewa kandoni mwa kikao cha 13 cha kamati ya kimataifa ya mkataba kuhusu ulinzi na uchagizaji wa tamaduni tofauti kinachofanyika mjini Paris Ufaransa.

Akizungumzia tangazo hilo Bi. Azoulay amesema “Ni muhimu kwa sekta ya filamu kufanya sauti za Afrika zisikike ili kusaidia kuibua ukuaji wa tamaduni tofauti , kuweka mawazo mapya na hisia, na kuhakikisha kwamba wanawake kama watayarishaji wanachangia katika majadiliano muhimu ya kimataifa kwa ajili ya amani, utamaduni na maendeleo.”

Wanawake hao 10 watayarishaji wa filamu wenye umri wa kati ya miaka 21 hadi 35 kutoka Burkina Faso, Kenya, Senegal na Afrika Kusini watakuwa mafunzoni katika makazi ya Tawara katika mkoa wa Nara, kuanzia tarehe 29 Machi hadi 12 Aprili mwaka huu.

Watapatiwa mafunzo na Bi. Kawase na mtayarishaji filamu kutoka Senegal Fatou Kande Senghor. Mradi huo unaungwa mkono na serikali ya Japan na wakfu wa Japan.

Bi.Kawase anasema kwa upande mmoja “kuwa mwanamke ilifanya kuwa rahisi kwangu kuangalia kwa karibu mazingira yangu , sio kuwa katika ulingo au kuwa kinara, wanawake wanaweza kufanya mapinduzi mapya. Kwa upande wangu naanda vitu kutokana na vyanzo vyangu mwenyewe. Naamini kuna kitu cha kimataifa katika uzoefu wangu binafsi”

Watayarishaji hao wa filamu

Watayarishaji hao 10 wa filamu vijana waliotanmgazwa leo ni :

Mayowa Bakare, Mwandishi wa filam wa Nigeria na muongozaji msaidizi. Na amaamini kwamba "Hakuna hadithi za kutosha kuhusu wanawake zinazoelezewa na wanawake. Nitachunguza simulizi tofauti kwa hadithi tunazosimulia sie wenyewe.”

Okule Dyosopu, mkurugenzi wa filamu wa Afrika Kusini, mwanzilishi wa kampuni huru ya utayarishaji wa filamu.Anasema  "Wanawake ndio siri kubwa iliyowekwa vizuri zaidi katika tasnia ya filamu. Mimi ndiye mabadiliko ninayotaka kuyaona. "

Awa Gueye, mkurugenzi wa filamu tano kutoka Senegal. "Leo, tunashikilia sana umuhimu muonekano. Ninataka kuuchukua uzuri kwa aina tofauti, uzuri katika kufungua na kukubali wengine. "

Joan Kiragu, mshindi wa tuzo ya utengenezaji filamu kutoka Kenya. Anasema "Makaazi haya yanatoa jukwaa la kimataifa kwa sauti za wanawake. Nitakuwa balozi anayesisitiza na kusongesha mbele ajenda wakati huohuo nikitoa hadithi ambazo ni za muhimu.

Uren Makut, mkurugenzi na mtengenezaji wa filamu kutoka Nigeria, ni mwanzilishi wa kituo cha mafunzo kwa watengenezaji chipukizi wa  filamu. Anasema "Wanawake daima wamekuwepo katika ulingo wa utengenezaji wa filamu lakini wamekuwa nyuma ya pazia. Ni wabunifu sana na watafanya vitu vya ajabu wanapotiwa moyo.”

Lydia Matata, mtengenezaji wa filamu kutoka Kenya, mwandishi  wa hadithi na mwandishi wa habari. “Utengenezaji wa filamu, kama maisha, hutoa mafunzo kila siku. Nataka ujasiri kwamba kile ninachochunguza kupitia kazi yangu kama mtayarishaji wa wa kike wa Kiafrika iwe nzuri na muhimu kama wenzangu mahali pengine. "

Fama Reyanne Sow, muongozaji wa filamu kutoka Senegal na mwandishi wa michezo ya kuigiza ya filamu. "Nataka kuandaa kundi la wahusika wa filamu wenye nguvu ambao ni wanawake ili vijana wa Senegal wawe na mashujaa wanaowapendeza."

Delphine Yerbanga, muongozaji na mtayarishaji wa vipindi vya runinga ya umma ya Burkina Faso. "Makazi haya yatakuwa mchakato wa ubunifu ambao unaweza kunionyesha jinsi ya kukuza wazo na kuunda filamu inayoonekana."

Thishiwe Ziqubu, muongozaji na mwanzilishi wa kampuni ya uandaaji wa filamu nchini Afrika Kusini. "Sitaki tu kuwa mtengenezaji wa filamu wa Afrika Kusini, bali msanii wa kimataifa ambaye lazima apanue mtazamo wake wa ulimwengu ili kuandaa kazi ambayo inayovuka mipaka."

Floriane Zoundi, muongozaji na mwandishi wa vipindi vya televisheni huko Burkina Faso. "Wanasema muongozaji wa filamu ni kama muongozaji wa okestrawa. Ninataka kupata ujuzi mpya, kuangalia wengine wakifanya kazi, na kusikiliza na kushiriki ana mawazo na watu wa rika langu. "

 Waandaaji hao wa filamu watatayarisha miradi mbalimbali ya filamu na kushiriki katika darasa maalum la kupigwa msasa wa uandaaji wa filamu, watarekedi na kujadili kuhusu kazi walizozifanya.

Na kisha wataalikwa kuwasilisha kazi zao kwenye tamasha lijalo la kimataifa la filamu la Nara tarehe 18-22 Septemba 2020.

Wanawake na Afrika ni vipaumbele viwili vya kimataifa kwa UNESCO . Darasa la filamu linatoa mchango mkubwa katika kuendeleza taaluma ya uaandaaji wa filamu  na maendeleo ya wanawake katika tasnia hiyo na kupanua wigo wa filamu za Afrika.