Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara mtandaoni ni fursa kwa masoko ya nje:UNCTAD

Mtu anarambaza kupitia mitandao ya kijamii.
World Bank/Simone D. McCourtie
Mtu anarambaza kupitia mitandao ya kijamii.

Biashara mtandaoni ni fursa kwa masoko ya nje:UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Burkina Faso, Senegal na Togo wanahitaji mageuzi makubwa ya miundombinu yao na mifumo ya kisheria ili kufaidika na biashara ya mtandao yaani e-commerce, tafiti mpya zilizofanywa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara UNCTAD kuhusu nchi za Magharibi mwa Afrika zimeeleza.

Wawakilishi wa nchi hizo tatu wanakutana nchini Burkina Faso kuangalia mstakabali wao katika biashara kwa njia ya mtandao na kinachotakiwa kufanyika kuzitambua na kutumia fursa hiyo.

Ripoti zitawasilishwa mjini Ouagadougou, Burkina Faso, tarehe 9–10 Oktoba katika warsha ya kikanda kuhusu biashara kwa njia ya mtandao iliyoandaliwa na UNCTAD na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS.

“Tafiti zilizofanywa na UNCTAD zinaonesha kuwa miradi ya mageuzi makubwa inahitajika kwa Burkina Faso, Senegal na Togo ili kutumia kikamilifu fursa za maendeleo zinazoletwa na biashara ya mtandaoni na kwamba itahitajika utayari wa serikali. UNCTAD iko hapa kusaidia. Huu ni mkakati wa nipe nikupe, ambao unatakiwa kufanyika kwa kuwa biashara mtandaoni hivi sasa ni lango la masoko ya nje” naibu katibu mkuu wa UNCTAD Isabelle Durant anasema.

Warsha hii ni hatua ya kwanza katika maandalizi ya mpango wa kikanda na itazinduliwa na Bi. Durant katika uwepo wa kamishna wa kilimo, raslimali za maji na mazingira wa ECOWAS, Jonas Gbian na Daouda Ouedraogo, mwakilishi wa wizara ya biashara, viwanda na kazi za mikono wa Burkina Faso.

Huku ikizingatia hali mahususi za kila nchi, tathimini za UNCTAD zimeonyesha vikwazo ambavyo nchi zote zinakabiliana navyo.

Ingawa kila moja imejitolea kujenga mazingira ya kidijitali, hakuna ambayo imeweka wa biashara za mtandaoni. Na kiwango cha chini cha upatikanaji wa mtandao wa intaneti na ubora wa huduma, kutokana na ukosefu wa ushindani katika sekta ya mawasiliano ya simu, ni kikwazo kwa ukuaji wa kidijitali.

Miundombinu dhaifu na yenye gharama, na mipango ya huduma ambazo hazijaunganishwa vizuri na waendeshaji, zinafanya bidhaa zinazouzwa au kununuliwa kuwa vigumu kufika kituo cha mwisho.

Pia Burkina Faso, Senegal na Togo zote zinakabiliana na tatizo la  upatikanaji wa fedha za kuunga mkono biashara ya mtandaoni.

UNCTAD imekuwa ikifanya tathimini ya biashara mtandaoni kwa nchi zinazoendelea tangu mwaka 2016, ikitambua kuwa watunga sera watatakiwa kwenda haraka ikiwa nchi maskini zinataka kwenda na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi.