Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya raia na wimbi la watu kutawanywa lazima vikome Syria:UN

Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi
UNICEF/UN0277723/Souleiman
Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi

Mauaji ya raia na wimbi la watu kutawanywa lazima vikome Syria:UN

Amani na Usalama

Mashambulizi ya angani na ardhini ya jimbo la Idlib Kaskazini Magharibi mwa Syria yanasababisha wimbi kubwa la watu kutawanywa na Maisha ya raia kupotea na haya ni madhila ambayo hayastahili na yanapswa kukomeshwa sasa amesema Geir Pedersen mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo.

Mark Lowcock mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa(OCHA) ambaye pia ametoa taarifa kwenye Baraza la Usalama ameelezea kinachoendelea Syria kuwa ni “zahma kubwa ya kibinadamu inayosababishwa na operesheni za kijeshi zinazoendelea.”

Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 30 kusaidia

Mkuu huyo wa OCHA ametangaza kwamba dola milioni 30 zimetolewa na mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF ili kusaidia mara moja katika mahitaji ya dharura ya malazi na huduma zingine muhimu kwa maelfu ya raia wanaolipa gharama ya janga la kibinadamu linaloendelea Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Lowcock amesema “Tumeona picha katika mji mmoja baada ya mwingine wakati magari yakijipanga kila kona watu wakijaribu kukimbia. Watu ambao wamehama hawawezi kupata malazi, maelfu wamejihifadhi kwenye mashule, misikiti na majengo ambayo hayajakamilika. Na wengi wanaishi katika mahema yaliyowekwa kwenye tope wakikabiliwa na upepo mkali, mvua na baridi kali.”

Fedha hizo zlilizotolewa na CERF zitasaidia kutoa malazi na huduma nyingine muhimu wakati huu wa msimu wa baridi Kali.

Kwa ushirikiano wa kimataifa suluhu haishindikani

Bwana Pedersen ameainisha kiwango cha operesheni za kijeshi katika eneo hilo ambazo zinajumuisha mashambulizi ya anga na ardhini katika eneo la Idlib ambayo yanafanywa na serikali ya Syria, mapigano baina ya vikosi vya Syria na vya Uturuki na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Hayat Tahrir al-Sham na makundi mengine yenye silaha.

Licha ya maombi kadhaa yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa kutaka pande zote kusitisha uhasama, mamia ya raia wameuawa katika miezi miwili iliyopita huku wengine zaidi ya nusu milioni wakitawanywa na watu wa kawaida wakijihidi kupuuzwa na kutelekezwa amesema mwakilishi huyo.

Ameonya kuwa “Hakuna suluhu yoyote ya kijeshi katika vita vya Idlib ambavyo vinatisha kuwa ni vya umwagaji damu mkubwa na vya muda mrefu kwenye mpaka wa Uturiki vikiwa na athari kubwa na mbaya kwa raia.”

Ushirikiano wa kimataifa na muafaka wa kusitisha uhasama vinaweza kuleta utulivu na mwakilishi huyo maalum amesema ataendelea kutroa shinikizo kwa wadau wakubwa katika vita hivyo kuhusu wajibu wao wa kufuata njia tofauati badala ya vita.

Amekumbusha kwamba wajumbe 15 wa Baraza la Usalama ambao waliafikiana bila kupingwa kuhusu azimio namba 2245 ambalo linaweka bayana kuhusu “Usitishaji mapigano nchi nzima sambamba na mtazamo wa ushirikiano ili kukabiliana na ugaidi na kwa kuheshimu kikamilifu uhuru wa Syria na mchakato wa kisiasa unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.