Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 520,000 wamefurushwa makwao Syria kwa miezi miwili iliyopita:OCHA

Syria, jimbo la Al-Hasakeh Oktoba 11, 2019, wanawake waliofurushwa wakisafiri kwa njia ya bara bara.
WFP/Alan Ali
Syria, jimbo la Al-Hasakeh Oktoba 11, 2019, wanawake waliofurushwa wakisafiri kwa njia ya bara bara.

Zaidi ya watu 520,000 wamefurushwa makwao Syria kwa miezi miwili iliyopita:OCHA

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa na washirika wake wa masuala ya kibinadamu wanaongeza juhudi za kukabiliana na mahitaji ya maelfu ya watu waliojikuta katikati ya machafuko Kaskazini Magharibi mwa Syria

Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, tangu Desemba mosi mwaka jana katika kipindi cha miezi miwili zaidi ya watu 520,000 wamefurushwa makwao na machafuko wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Amesema wengi wa watu hao wameondoka bila chochote zaidi ya nguo walizovaa na wanahitaji msaada wa haraka wa malazi, chakula, maji, vifaa vya usafi na kujisafi, huduma za afya, elimu ya dharura na ulinzi, na watu wengine 280,000 zaidi wako katika hatari kubwa ya kutawanywa katika maeneo ya mijini endapo operesheni ya kijeshi itaendelea. Msemaji huyo Jens Laerke amesema ’’Jumuiya ya misaada ya kibinadamu iko na mipango ya operesheni kushughulikia mahitaji ya takriban watu 800,000 Kaskazini Magharibi mwa Syria katika muda wa miezi sita. Mahitaji ya mpango huu n idola milioni 336.”

Mashambulizi ya vifaru na makombora yamesababisha madhila makubwa kwa raia na jumla ya watu 1500 wamepoteza maisha katika kipindi hicho kifupi. Bwana Laerke ameongeza kuwa wamepokea ujumbe kutoka wafanyakazi wa OCHA eneo hilo ambao wanasema “Hakuna mahali salama Idlib, mabomu yanaanguka kila mahali. Hata wale wanaokimbia mstari wa mbele wa mapambano hawako salama, ni wimbi la watu wanakwenda kila kona wakati mashambulizi ya anga na makombora yakiendelea kwa mizi miwili iliyopita. Changamoto kubwa ni malazi, maelfu ya watu wanapata hifadhi mashuleni na misikitini, wengi wako katika mahema wakipigwa na upepo mkali, mvua na baridi Kali.”

Pia amesema wameshitushwa sana na kuendelea kwa operesheni za kijeshi Kaskazini Magharibi mwa Syria ambako raia milioni 3 wamekwama katika uwanja wa mapambano, na nusu yao wakiwa ni watoto na wengine wengi ni wazee.