Tuko tayari kusaidia kiufundi katika mlipuko wa corona:IOM

31 Januari 2020

Wakati hofu ikiendelea kutanda kuhusu idadi ya visa vilivyoripotiwa kutokana na mlipuko wa virusi vipya vya Corona na pia kusambaa kwake katika nchi 18 hivi sasa, shirika la umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema liko tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa serikali likishirikiana na shirika la afya ulimwenguni WHO ili kuwawezesha watu kusafiri katika njia salama kiafya na kusaidia utekelezaji wa hatua za afya za kijamii ili kuhakikisha athari ndogo katika jamii na uchumi.

Kwa mujibu wa takiwmu zilizotolewa leo Ijumaa na WHO kuna jumla ya visa 9692 vilivyobainiwa vya virusi vya Corona na vifo 213. Jacqueline Weekera mkurugenzi wa IOM idara ya afya na uhamiaji amesema “wakati visa vipya vinaendelea kuripotiwa kila siku bado kuna mengi yanayopaswa kueleweka kuhusu virusi hivi, lakini kilichobayana ni kwamba watu kusafiri ni hali halisi na tunapaswa kutafuta njia ndani ya uhalisia huo kuhakikisha kila mtu yuko salama na wenye afya, huku tukidhibiti usumbufu na athari za kijamii na kiuchumi”

Dharura ya kimataifa ya afya

Masafisa wa afya wa kimataifa waliokuwa wamekusanyika mjini Geneva jana kwa kikao kuhusu virusi vya Corona wwalitangaza kwamba sasa virusi vya Corona ni dharura ya afya ya kimataifa inayotia hofu(PHEIC), wakiainisha haja ya uratibu wa kimataifa wa hatua za kukabiliana na virusi hivyo.

Hata hivyo “kamati hiyo ya wataalam haikupendekeza vikwazo vyovyote vya safari au biashara kwa taarifa zilizopo.”

Kutokana na sheria za kimataifa za afya ingawa vikwazo vya safari za kimataifa ingeonekana kuwa ndio kitu sahihi cha kufanya, hii sio kitu ambacho kwa kawaida hupendekezwa kutokana na usumbufu wa kijamii unaoweza kusababishwa na vikwazo hivyo.

Kwa hivyo IOM na WHO wanapendekeza kujikita zaidi na maandalizi na hatua za kuvikabili virusi hivyo. Kaimuafisa huyo wa IOM amesema “IOM ina utaalam wa kuzisaidia nchi kutekeleza maandalizi ya lazima na hatua za kuchukua ikiwemo uratibu mipakani, masuala ya wahamiaji na elimu, ujumuishwaji wa jamii zinazohama, kukomesha mnyororo wa maambukizi. IOM imeunda mtandao wa kijamii kwa ajili ya wahamiaji na watu wanaosafiri kote duniani ambao unaweza kutumika kwa kutoa taarifa za hatariikiwa ni hatua muhimu katika kuzisaidia familia kufahamishwa na kujilinda”

Hatua zinazochukuliwa

Miongoni mwa maandalizi na hatua za kukabiliana na mlipuko huo ambazo IOM na washirika wake wamekuwa wakizifanya ni kuzisaidia serikali kuhusu suala la afya na uhamiaji kwa kutoa mafunzo, kuunda muongozo, kuboresha viwango vya usafi wa maeneo kadhaa na kusaidia kuandaa muongozo wa kutumiwa katika viwanja vya ndege, maeneo ya mipakani na kwenye bandari.

Kwa mfano mapema mwezi huu IOM kwa kushirikiana na idara ya Marekani ya kudhibiti magonjwa (CDC) waliisaidia serikali ya Senegal kuendesha zoezi la mfano la kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa na udhibiti kwenye uwanja wa ndege wa Dakar ikiwa ni tahadhari ya endapo dharura kubwa ya afya ya umma itazuka.

Mbali ya kutoa msaada na muongozo IOM imerejea kusisitiza haja ya ujumuishaji na kutoa wito kwa nchi kuhakikisha kwamba wahamiaji na wasio raia wanajumuishwa pia katika taarifa na mipango ya afya ya umma.

Kwa kuzingatia misingi ya kimataifa ya afya kamati ya dharura ya WHO “imeonya juu ya hatua ambazo zitachagiza unyanyapaa na ubaguzi”

Dkt. Nennete Motus mkurugenzi wa IOM kanda ya Asia-Pasifiki amesisitiza kwamba “Taarifa ni muhimu na pia ni muhimu kwamba tunafanyakazi pamoja kuzuia unyanyapaa katika safari za kimataifa.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter