Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msiwanyanyapae watu wa asili ya Asia kwa sababu ya corona-UN

Wahudumu wa ndege wakiwa wamejikinga baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Shenzhen Bao'an nchini China
Man Yi
Wahudumu wa ndege wakiwa wamejikinga baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Shenzhen Bao'an nchini China

Msiwanyanyapae watu wa asili ya Asia kwa sababu ya corona-UN

Afya

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutowanyanyapaa na kuwabagua watu wenye asili ya bara Asia kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya corona ambavyo vimeathiri kwa kiasi kikubwa China na nchi nyingine.

Matukio kadhaa ya ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wenye asili ya Asia yameripotiwa katika baadhi ya maeneo duniani. Watu wa asili ya Asia wameonekana kuwa waathirika wa maoni ya unyanyapaa na vitendo vya kibaguzi.

"Katika kipindi hiki cha wasiwasi ulioongezeka, lazima tuepuke unyanyapaa na ubaguzi, na tuendelee kuwa na umoja na huruma," Katibu Mkuu wa UN António Guterres amesema leo kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa Twittter.

Ijumaa wiki iliyopita, tayari Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) nayo ilikuwa imelipigia kelele suala hili kupitia Twitter ikisema, “Inaeleweka kushtushwa na virusi vya corona. Lakini hakuna woga wowote unaoweza kuhalalisha ubaguzi na ubaguzi dhidi ya watu wa asili ya Asia,"

Jumatano iliyopita, WHO ilitangaza virusi hivyo vya corona kuwa ni dharura ya afya kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus alinukuliwa akisema "kwa watu wa China na kwa kila mtu duniani kote ambao wameathirika na virusi hivi, jua kuwa dunia iko pamoja nanyi.“

Hadi kufikia hii leo , mlipuko huo umeshasababisha vifo vya watu 361 nchini China na kifo kimoja kimeripotiwa nchini Ufilipino, na visa vyote kwa ujumla vikiwa vimefika 17,389.