Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia haitaangamia, lakini sisi ndio tutaangamia-Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kwenye kongamano la kila mwaka la kimataifa la uchumi.
World Economic Forum/Boris Baldinger
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kwenye kongamano la kila mwaka la kimataifa la uchumi.

Dunia haitaangamia, lakini sisi ndio tutaangamia-Antonio Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaambia viongozi wa biashara katika Jukwaa la Uchumi Duniani,  hii leo mjini Davos, Uswisi kwamba ikiwa mataifa makuu ya viwanda hayatapunguza uzalishaji wao wa gesi chafu basi ulimwengu uko mashakani katika enzi hii ya mabadiliko ya tabianchi.

Akiongea kwenye ukumbi huo  Guterres alisema, "ni muhimu sana kutambua kwamba mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwetu sote, na kwamba mabadiliko ya tabianchi yanazidi kwa kasi kuliko sisi.”

Ameongeza kwamba sayari inastahimili na kwa hivyo haitaangamia,“katika karne chache zijazo na milenia, tutaona sayari ikizunguka jua. Kitakachoharibiwa ni uwezo wetu wa kuishi katika sayari hii. Tutaangamizwa na mabadiliko ya tabianchi, sio sayari. Na hii itakuwa ishara dhahiri kwamba tunahitaji kubadilisha mwenendo.”

Bwana Guterres ameshuhudia kwamba wakati nchi ndogo zinazoendelea na Jumuiya ya Ulaya zimejitolea kufikia kupunguza gesi za kaboni ifikapo mwaka 2050, wazalishaji wakubwa wa gesi hizi bado hawajachukua hatua.