Iwapo mazungumzo hayawezekani Venezuela, tunafanya nini? Ahoji Guterres

24 Januari 2019

Ghasia zikiendelea kurindima huko Venezuela kutokana na mvutano baada ya kuapishwa kwa Rais Nicolas Maduro huku baadhi ya mataifa na wananchi wakimuunga mkono kiongozi wa  upinzani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake juu ya hali hiyo.

Taarifa kupitia msemaji wake iliyotolewa jijini New York, Marekani imemnukuu akielezea hofu yake kutokana na ripoti za vifo na majeruhi akitaka uchunguzi wa kina na wa wazi kuhusu matukio hayo.

Mapema leo akizungumza huko Davos, Uswisi kwenye mahojiano ya moja kwa moja kupitia mtandao wa Facebook, Bwana Guterres amesema ni wazi kuwa nchi huru zina haki ya kuamua kile inachotaka juu ya kutambua serikali akisema hiyo ni haki yao.

Hata hivyo amesema, “Kile kinachotutia hofu zaidi na kinachoendelea Venezuela ni machungu ambayo wanapitia wananchi wake. Watu wengi wamekimbia nchi hiyo, kutokana na hali ngumu ya uchumi na siasa kuleta mgawanyiko mkubwa.”

Amesema matumaini yake ni kwamba mazungumzo yanawezekana na ni lazima kuepuka mvutano zaidi ambao unaweza kusababisha mzozo utakaokuwa janga kubwa kwa wananchi wa Venezuela na eneo zima la Amerika ya Kusini.

“Iwapo mazungumzo hayawezekani, je tunafanya nini? Namaanisha, katika mazingira yoyote yale duniani, hata katika mazingira magumu zaidi, lazima tuweke shinikizo la kufanyika kwa mazungumzo,” amesema Guterres.

Ametolea mfano Yemen ambako mataifa mengine yanahusika kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya, na kuwa janga baya zaidi la kibinadamu duniani akisema kuwa watu wanaweza kudai ya kwamba mazungumzo hayawezekani.

Katibu Mkuu amesema “tulishiriki kwa dhati na tuliweza kufanikisha mazungumzo na tumeshuhudia maendeleo. Kwa hiyo mazungumzo ni msingi wa kutatua matatizo ya kibinadamu.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud