Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za sasa duniani ni za pamoja lakini utatuzi “segemnege”-  Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) wakati akihutubia jukwaa la kiuchumi duniani, WEF, huko Davos Uswisi. Kulia kwake ni rais wa jukwaa hilo Børge Brende
WEF/Benedikt von Loebell
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) wakati akihutubia jukwaa la kiuchumi duniani, WEF, huko Davos Uswisi. Kulia kwake ni rais wa jukwaa hilo Børge Brende

Changamoto za sasa duniani ni za pamoja lakini utatuzi “segemnege”-  Guterres

Masuala ya UM

Jukwaa la uchumi duniani likiendelea huko Davos nchini Uswisi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameweka bayana changamoto zinazokabili dunia hivi sasa akisema jawabu muhimu ni ushirikiano wa kimataifa ambao chombo anachoongoza ndio msingi wake. Assumpta Massoi na taarifa zaidi. 

Guterres amesema uchumi wa dunia unasuasua, giza nene limezingira dunia kiuchumi, kisiasa na kijamii na kutilia shaka mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 

Kama hiyo haitoshi, utandawazi unazidi kuongeza ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuengua watu kwenye mwelekeo wa usawa  huku maendeleo ya tekneolojia nayo yakichagiza karaha badala ya raha.

“Tuko katika dunia ambamo kwayo changamoto za dunia zinahusiana lakini suluhu kila mtu anafanya kivyake. Iwapo hili halitabadilishwa basi ni kichocheo cha janga.”

UN Kiswahili Social Media
Davos!

Katibu Mkuu amesema hakuna nchi peke yake inaweza kukabili hali ya sasa kwa hiyo Umoja wa Mataifa vipaumbele vyake ni vitatu ikiwemo..

“Kudhihirisha kwa wale wote wanaopinga ushirikiano wa kimataifa kuwa tunawajali, kudhihirisha kwa wale wote walioachwa nyuma kuwa mawazo,  será na mipango yetu inalenga kuwawezesha kutatua matatizo yao.”

Kuhusu Venezuela ambako hivi sasa kuna vuta ni kuvute baada  ya Rais Nicolas Maduro kuapishwa na baadhi ya nchi na wananchi kuunga mkono kiongozi wa upinzani, Katibu Mkuu amesema nchi huru zina haki ya  kuamua kile ambacho inaona kinafaa lakini Umoja wa Mataifa una hofu kuwa kinachoendelea kinaleta machungu kwa raia wa kawaida.