Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la pengo la usawa linaathiri theluthi mbili ya dunia:UN

Bango la ripoti ya maswala ya kijamii duniani.
UN
Bango la ripoti ya maswala ya kijamii duniani.

Ongezeko la pengo la usawa linaathiri theluthi mbili ya dunia:UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Pengo la usawa duniani linaongezeka kwa zaidi ya asilimia 70 ya watu wote duniani na hivyo kuongeza hatari ya migawanyiko na kuathiri maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Lakini ongezeko hilo linaweza kudhibitiwa na kushughulikiwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo Jumanne.

Ripoti hiyo “ Ya masuala ya kijamii duniani 2020” iliyochapishwa na idara ya uchumi na masuala ya kijamii ya Umoja wa Mataifa DESA inaonyesha kwamba pengo katika masuala ya kipato limeongezeka katika nchi zilizoendelea na baadhi ya nchi za kipato za kati ikiwemo China ambayo uchumi wake ndio unaokuwa kwa kasi kubwa hivi sasa duniani.

Changamoto hiyo imesisitizwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ambaye amesema “dunia inakabiliwa na ukweli kwamba pengo la usawa ni kubwa ambapo uchumi unayumba, hofu ya kutokuwa usawa na ajira vimesababisha maandamano makubwa katika nchi zilizoendelea na kwa zile zinazoendelea. Tofauti za kipato na ukosefu wa fursa vinasababisha mzunguko wa kutokuwepo kwa usawa , kunazusha taharuki na kutoridhika katika vizazi vyote”.

Wachache ndio wanaofaidika zaidi

Utafiti wa ripoti hiyo umeonyesha kwamba matajiri kuliko wote ambao ni asilimia moja ya watu duniani ndio wanaufaika wakubwa katika uchumi wa kimataifa unaobadilika wakijiongezea pato la utajiri wao tangu mwaka 1990 na 2015, huku kwa upande mwingine wa mizani asilimia 40 ya walio chini walipata robo tu ya pato la matajiri hao katika nchi zote zilizofanyiwa utafiti.

Ripoti inasema moja ya athari za pengo la usawa katika jamii ni kuzorota kwa ukuaji wa uchumi. Katika jamii ambazo hazina usawa, zenye pengo kubwa katika masuala kama ya huduma za afya na elimu, watu wako katika asilimia kubwa ya kuendelea kukwama kwenye mzunguko wa umasikini kwa vizazi hadi vizazi.

Miongoni mwa nchi kwa mujibu wa ripoti tofauti ya kiwango cha wastani cha kipato inapungua wakati China na nchi zingine za Asia zikisukuma ukuaji wa uchumi wa kimataifa. Hata hivyo ripoti imeonya kwamba bado kuna tofauti kubwa baina ya nchi na kanda tajiri na masikini. Mathalani wastani wa kipato Amerika Kaskazini ni mara 16 zaidi ya watu walioko Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.

Wanafunzi wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam Tanzania
World Bank / Sarah Farhat
Wanafunzi wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam Tanzania

Mambo makubwa manne yanayochochea pengo la usawa

Ripoti imemulika masuala manne makubwa yanayochochea ongezeko la pengo la usawa duniani kuwa ni ubunifu wa teknolojia, mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa miji na uhamiaji wa kimataifa.

Imesema wakati ubunifu wa teknolojia unaweza kusaidia ukuaji wa uchumi , kutoa fursa mpya katika masuala ya huduma za afya, elimu, mawasiliano na uzalishaji, pia kuna ushahidi unaoonyesha kwamba unaweza kusababisha ongezeko la pengo la mishahara na kutawanya wafanyakazi.

Ripoti imeongeza kuwa maendeleo ya haraka katika masuala ya baolojia na vinasaba, lakini pia roboti na akili bandia (AI) vinabadolisha jamii kwa kasi.

Teknolojia mpya zinauwezo wa kutokomeza kabisa aina fulani za ajira , lakini vivyohivyo inaweza kuzalisha ajira mpya na ubunifu.

Kwa sasa lakini ripoti inasema wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu wananuafaika na faida za kile kinachoitwa “Mapunduzi ya nne ya viwanda” huku wale wenye ujuzi mdogo na wa wastani wanaojihusisha na mfumo uliozoeleka wa kazi za mikono zinazotambulika wanashuhudia fursa zao zikipungua.

Fursa katika zahma

Kama ilivyoonyesha ripoti ya hali ya uchumi duniani kwa mwaka 2020 wiki iliyopita, mabadiliko ya tabianchi yana athari mbaya kwa ubora wa maisha, na watu wasiojiweza ndio wanaobeba gharama kubwa ya mmomonyoko wa mazingira na matukio yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mabadiliko ya tabianchi kwa mujibu wa ripoti ya masuala ya kijamii duniani yanzifanya nchi masikini duniani kuwa masikini zaidi na yanaweza kubadili hatua zilizopigwa katika kupunguza pengo la usawa miongoni mwa nchi.

Endapo hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kama inavyotarajiwa kutakuwa na kupoteza ajira katika sekta za hewa ukaa kama vile viwanda vya makaa ya mawe, lakini kuwa na uchumi wa kijani duniani kutasababisha ongezeko la ajira kwa ujumla kwa kuanzishwa ajira nyingi mpya kote duniani.

Kwa mara ya kwanza katika historia watu wanaishi mijini kuliko vijijini, mwenendo unaotarajiwa kuendelea katika miaka mingi ijayo. Ingawa miji inachagiza ukuaji wa uchumi kuna tofauti kubwa na vijijini kukiwa na maisha ya kitajiri sana na ya kimasikini sana.

Kiwango cha umasikini kinatofautiana baiana ya mji na mji hata ndani ya nchi moja, wakati miji inakuwa na kuendelea, baadhi ya miji imekuwa na pengo kubwa la usawa huku mingine pengo hilo likipungua.

Uhamiaji ishara tosha ya pengo la usawa duniani

Mwenendo wa nne ni uhamiaji wa kimataifa ukielezwa kama ni “Ishara tosha ya pengo la usawa duniani na chachu ya pengo hilo katika mazingira ya sasa”. Uhamiaji ndani ya nchi kwa mujibu wa ripoti unatabia ya kuongezeka kwani nchi zimeanza kuendelea na kukua kiviwanda na kuongezeka kwa wakazi wa nchi za kipato cha wastani kuliko cha chini wanahamia nje ya nchi.

Uhamiaji wa kimataifa unaonekana kufaidisha pande zote wahamiaji, nchi watokako kwa sababu ya kutuma pesa n anchi zinazowahifadhi. Wakati mwingine katika nchi ambako wahamiaji wanashinadana kupata kazi zenye ujuzi mdogo , mishahara inaweza kupunguzwa, kuongeza pengo la kutokuwepo na usawa, lakini endapo watatoa ujuzi ambao haupatikani kwa urahisi au kuchukua kazi ambazo wengine hawako tayari kuzifanya inawezekana kuwa na athari chanya katika tatizo la ajira.