Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi ndio kikwazo cha Maisha bora na kutoridhika duniani: WESP

Mazambara, Zimbabwe, ambapo mvua imeadimika, mwanamke anaonyesha sahani ya cicagas, moja wapo ya chaguzi za chakula wakati uwiano wa chakula wa WFP utakapomalizika.
WFP/Matteo Cosorich
Mazambara, Zimbabwe, ambapo mvua imeadimika, mwanamke anaonyesha sahani ya cicagas, moja wapo ya chaguzi za chakula wakati uwiano wa chakula wa WFP utakapomalizika.

Mabadiliko ya tabianchi ndio kikwazo cha Maisha bora na kutoridhika duniani: WESP

Tabianchi na mazingira

Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, kuendelea kwa pengo la usawa, kuongezeka kwa mzigo wa madeni na ongezeko la viwango vya kutokuwa na uhakika wa chakula na utapiamlo vinaathiri ubora wa maisha katika jamii nyingi na kuchangia hali ya kutoridhika umeonya Umoja wa Mataifa hii leo katika ripoti yake ya hali ya uchumi duniani na matarajio mwaka 2020 (WESP).

Utafiti wa ripoti hiyo umebaini kwamba mwaka 2019 uchumi wa dunia ulikuwa wa asilimia 2.3 , ukiwa ni ukuaji wa kiwango kidogo na wa polepole katika kipindi cha muongo mmoja, huku matarajio yakionyesha kwamba ukuaji wa asilimia 2.5 yanawezekana kwa mwaka 2020. Lakini ripoti hiyo inasema matarajio hayo yanaweza kuingia doa kutokana na kuongezeka kwa mivutano ya biashara , changamoto za kifedha au kuendelea kwa mibvutano ya kisiasa ya kimataifa.

Kuhamia kwenye nishati safi na salama kunahitajika haraka

Mfumo wa gridi dogo la jua nchini Eritrea inaipa nguvu miji mbili ya vijijini na vijiji vinavyozunguka.
UNDP Eritrea/Elizabeth Mwaniki
Mfumo wa gridi dogo la jua nchini Eritrea inaipa nguvu miji mbili ya vijijini na vijiji vinavyozunguka.

Wataalam wa Umoja wa Mataifa walioandaa ripoti hiyo kwa pamoja wametoa wito wa kufanyika mabadiliko makubwa kwenye sekta ya nishati ambayo kwa sasa ndio chanzo kikuu cha takribani robo tatu ya utoaji wa gesi chafuzi ya viwandani duniani. Ripoti hiyo inaonya kwamba “endapo dunia itaendelea kutegemea mafuta ya kisukuku katika miaka michache ijayo , na utoaji wa hewa chafuzi katika nchi zinazoendelea ukifikia katika kiwango cha nchi zilizoendelea , basi utoaji wa hewa ukaa duniani utaongezeka kwa zaidi ya asilimia 250 na kuwa na uwezekano wa kuleta janga kubwa.” Waandishi wa ripoti hiyo wanaisitiza kwamba “Mahitaji ya nishati ya dunia ni lazima yatimizwe kwa kutumia nichati endelevu au inayojali mazingira ambayo itasaidia kuhakikisha faida za mazingira na afya kama vile kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa na kutoa fursa mpya za kiuchumi kwa nchi nyingi.”

Hata hivyo ripoti hiyo 2020 WESP imebaini kwamba haja ya kuhamia haraka kwenye nishati safi na salama inaendelea kutopewa uzito na kwamba nchi zinaendelea kuwekeza katika uchimbaji wa mafuta na gesi, na uzalishaji wa makaa ya mawe.

Wamesisitiza kwamba utegemezi huu wa mafuta ya kisukuku ni “maono ya muda mfupi” ambayo yanawaacha wawekezaji na serikali katika hatari ya hasara ya ghafla kutokana na bei za mafuta na gesi kubadilikabadilika, lakini pia kuchangia kuzorota kwa hali ya hewa kama ongezeko la joto duniani.  Ripoti hiyo imehitimisha kwamba “ Hatari zinazohusiana na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuwa changamoto kubwa na hivyo hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zinapaswa kuwa sehemu ya sera yoyote ya kila nchi.”

Ripoti pia imesema mikakati na teknolojia ya kuhamia katika uchumi safi ambao utatoa fursa ya kuwa na nishati endelevu nay a kutegemewa tayari ipo, lakini itahitaji utashi wa kisiasa na msaada wa umma. Na kushindwa kuchukua hatua kutaongeza kwa kiasi kikubwa gharama.

Asia inapiga hatua huku Afrika ikijikongoja

Mfanyikazi wa kike katika kiwanda cha uchapishaji mjini Kyoto, Japan.
ILO/Marcel Crozet
Mfanyikazi wa kike katika kiwanda cha uchapishaji mjini Kyoto, Japan.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ukanda wa  Asia Mashariki unaendelea kuwa ndio wenye uchumi unaokuwa kwa kasi huku uchumi wa Uchina ukikuwa katika kiwango cha asilimia 6.1 kwa mwaka 2019. Ingawa ukuaji huo unatarajiwa kupungua kidogo , bado China inashuhudiwa kuwa na uchumi unaopita kwingineko duniani katika kiwango cha asilimia 5.9 ifikapo mwaka 2021.

Ripoti inasema nchi zilizoendelea duniani zinashuhudia ukuaji mdogo na wa polepole , mfano Marekani ikitarajiwa kuhuhudia kushuka kwa ukuaji uchumi kutoka asilimia 2.2 kwa mwaka 2019  hadi asilimia 1.7 mwaka huu wa 2020.

Kwa nchi za muungano wa Ulaya uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 1.6 pekee ingawa hili ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka 2019 kwani uchumi ulikuwa kwa asilimia 1.4 tu. Kudorora kwa ukuaji wa uchumi katika maeneo yote hayo kunalaumu hali ya sintofahamu iliyotawala duniani. Na kwa upabnde wa Afrika bara hili linaendelea kuathirika na kudumaa kwa ukuaji wa uchumi. Theluthi moja ya nchi hizo zinazoendelea zinategemea bidhaa ikiwemo Angola, Nigeria na Afrika Kusini, kiwango cha wastani cha kipato leo hii kiko chini kuliko ilivyokuwa mwaka 2014 na katika nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara idadi ya watu wanaishi katika umasikini wa kupindukia au ufukara imeongezeka.

Changamoto kwa ajenda ya maendeleo

Ingawa ripoti inataraji kwamba mivutano ya kibiashara itatulia , uwepokano wa kuzuka tena ni mkubwa inaonya ripoti hiyo kwani mzizi wa kuzuka kwa mivutano hiyo bado haujashughulikiwa. Imeongeza kuwa kuendelea kudorora kwa ukuaji wa uchumi duniani kutafanya kuwa vigumu kufikia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu. Ajenda hiyo ambayo ni nguzo ya Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha mustakbali bora wa watu na sayari dunia inajumuisha ahadi za kutokomeza umasikini  na kuunda ajira bora na zenye hadhi kwa wote.

Katika uzinduzi wa ripoti hiyo WESP , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya juu ya uwezekano wa athari za kudorora kwa ukuaji wa uchumi akisema “Hatari zinaweza kuleta athari mbaya na za muda mrefu katika maratajio ya maendeleo. Pia zinatishia kuchagiza zaidi ongezeko la será za ubinafsi katika wakati ambao ushirikiano wa kimataifa unahitajika na ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote”

Ukiaji wa uchumi pekee hautoshi

Waandishi wa ripoti wamehitimisha kwamba haitoshi kujikita tu na ukuaji wa uchumi, kwa gharama yoyote na serikali ni lazima zihakikishe kwamba ukuaji huo ni jumuishi. “watunga sera wanapaswa kwenda mbele zaidi ya mtazamo finyu  wa kuchagiza ukuaji wa pando la taifa GDP na badala yake walenge kuboresha ustawi katika Nyanja zote za jamii” amesema Elliott Harris, mchumi mkuu wa Umoja wa Mataifa na msaidizi wa Katibu Mkuu katika masuala ya uchumi na maendeleo.

Ili kuboresha ustawi kwa wote Bwana. Harris amesisitiza umuhimu wa vipaumbele vya uwekezaji katika malengo ya maendeleo endelevu katika kuchagiza elimu, nishati sadidifu, kujenga mnepo wa miundombinu na kutoa wito kwa serikali kutoa msukumo katika athari za sera zao kuhusu mazingira na mgawanyo wa haki wa rasilimali ndani ya nchi zao.

Ripoti ya hali ya uchumi na matarajio duniani WESP ni nini?

Ripoti ya hali ya uchumi na matarajio duniani WESP , chapisho linalotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu hali iliyopo na mwenendo unaotarakjiwa katika uchumi wa kimataifa.

Ripoti hiyo hutolewa kila mwaka na idara ya uchumi na masuala ya kijamii ya Umoja wa Mataifa (UNDESA), Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara (UNCTAD), na kamati tano za kikanda za Umoja wa Mataifa

 (Afrika, Ulaya, Amerika Kusini na Caribbea, Asia na Pasifiki, na Asia Magharibi).