Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCTAD yasema uchumi wa dunia uko njiapanda

Wanaume wakipakua magunia ya vitunguu kutoka kwa lori huko Bamako, Mali, nchi inayoendelea isiyo na bandari. Ukosefu wao wa ufikiaji wa moja kwa moja kwa viungo muhimu vya biashara mara nyingi husababisha nchi zisizo na bandari kulipa gharama kubwa za us…
World Bank/Dominic Chavez
Wanaume wakipakua magunia ya vitunguu kutoka kwa lori huko Bamako, Mali, nchi inayoendelea isiyo na bandari. Ukosefu wao wa ufikiaji wa moja kwa moja kwa viungo muhimu vya biashara mara nyingi husababisha nchi zisizo na bandari kulipa gharama kubwa za usafiri na usafirishaji.

UNCTAD yasema uchumi wa dunia uko njiapanda

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa UNCTAD, imezindua leo ripoti yake kuu ya Biashara na Maendeleo ya mwaka 2023 ambayo inachunguza kuimarika kwa uchumi wa dunia na kutoa utabiri wa kinachotarajiwa. Ripoti inaeleza hatua za kisera zinazopaswa kuchukuliwa ili kulinda uchumi wa dunia kutokana na matatizo ya kimfumo ya siku zijazo.

Hii ni ripoti ambayo hutolewa kila mwaka ikitathimini mwenendo wa ukuaji wa uchumi kote duniani, changamoto zinazojitokeza na nini kifanyike ili kuhakikisha uchumi unaendelea kukua na kuepusha athari kubwa kwa nchi lakini pia kwa Dunia nzima.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi safari hii imeonya kwamba uchumi wa Dunia unadorora na kuna tofauti kubwa za ukuaji wa uchumi huo miongoni mwa nchi na kanda duniani. 

Inasema “Ukuaji wa uchumi wa dunia unatarajiwa kupungua kutoka asilimia 3 mwaka jana hadi asilimmia 2.4 mwaka huu huku kukiwa na dalili chache za kuimarika tena mwaka ujao.”

Hivyo imeweka bayana kwamba “Uchumi wa dunia uko katika njia panda.”

Ripoti hiyo ya UNCTAD imeendelea kueleza kwamba “Njia tofauti za ukuaji uchumi, kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, kukua kwa hali ya kujikita na masoko na mzigo wa madeni vinahatarisha mustakabali wake wa uchumi wa dunia.” 

Mathalani ripoti imesema wakati nchi zilizoendelea kama Marekani, Uchina na nyinginezo za Ulaya zikijaribu kujikwamua kiuchumi kutokana na athari za janga la COVID-19 katika nchi zinazoendelea mchanganyiko wa viwango vya riba vinavyoongezeka, kudhoofika kwa sarafu zao na ukuaji duni wa mauzo ya nje vinabana nafasi ya kifedha inayohitajika kwa serikali kutoa huduma muhimu, na kubadilisha mzigo unaokua wa huduma ya madeni kuwa changamoto ya maendeleo inayojitokeza.

Takriban watu bilioni 3.3  karibu nusu ya binadamu wote duniani sasa wanaishi katika nchi ambazo hutumia zaidi fecha kwa ajili ya malipo yenye riba ya madeni kuliko katika huduma za elimu au afya.

Na nchi ambazo zimeathirika zaidi ni nchi zinazoendelea zenye kipato cha chini au ambazo zilianza kupata masoko ya mitaji ya kimataifa baada ya msukosuko wa kifedha duniani.

Kwa mantiki hiyo UNCTAD inatoa wito wa “Kutaka mageuzi ya kitaasisi katika usimamizi wa fedha duniani, sera za kiutendaji zaidi za kukabiliana na mfumuko wa bei, ukosefu wa usawa, madeni katika nchi na uangalizi thabiti wa masoko muhimu ili kufikia uthabiti wa kifedha, kuongeza uwekezaji wenye tija na kuunda nafasi bora za kazi.

Kusoma zaidi bofya hapa.