Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto watano wauawa na maroketi Idlib:UNICEF

Takribaini watoto 26,000 wenye umri wa kati ya miaka 3-17 kambini Al Hol kwenye jimbo la Hasakeh nchini Syria hawajaenda shuleni kwa miaka kadhaa kutokana na vita na ukimbizi na sasa wanahitaji huduma ya elimu.,
© OCHA/Hedinn Halldorsson
Takribaini watoto 26,000 wenye umri wa kati ya miaka 3-17 kambini Al Hol kwenye jimbo la Hasakeh nchini Syria hawajaenda shuleni kwa miaka kadhaa kutokana na vita na ukimbizi na sasa wanahitaji huduma ya elimu.,

Watoto watano wauawa na maroketi Idlib:UNICEF

Amani na Usalama

Wakati mwaka mpya ukianza na vita nchini Syria vikikaribia mwaka wa 10, hali kwa watoto wengi hususan walioko Kaskazini Magharibi mwa nchi ni mbaya sana

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF Henrietta Fore “ni jana tu siku ya mwaka mpya ambapo watoto watano wenye umri wa kati ya miaka 6 na 13 wameuawa wakati maroketi yalipoanguka kwenye shule ya msingi mjini Sarmin kwenye jimbo la Idlib.”

Ameongeza kuwa siku ya mwaka mpya inapaswa kuwa “siku ya matumaini na wakati wa kutafakari kusonga mbele katika mwaka unaofuata. Kwa familia nchini Syria matumaini yoyote mara nyingi huzimwa na mashafuko na simanzi.”

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kwamba kila siku karibu Watoto 4500 wanalazimika kukimbia makwao huku wengi wameshatawanywa mara kadhaa. Takriban Watoto 140,000 wametawanywa katika wiki tatu zilizopita pekee kwa sababu ya machafuko makubwa ndanina katika viunga vya mji wa Idlib Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Mashambulizi dhidi ya raia na hali mbaya ya hewa

Shule ya msingi katika mitaa ya Hujjaira, Damascus, Syria ikiwa imeharibiwa kutokana na vurugu za mara kwa mara katika katika eneo hilo.
UNICEF/M. Abdulaziz
Shule ya msingi katika mitaa ya Hujjaira, Damascus, Syria ikiwa imeharibiwa kutokana na vurugu za mara kwa mara katika katika eneo hilo.

 

Bi. Fore amesema “Mashambulizi katika miundombinu ya msingi ya raia inayotoa huduma kwa watoto kama shule na hospitali yamekuwa kama ada. Mwaka 2019 Umoja wa Mataifa ulithibitisha mashambulizi 145 katika shule na mashambulizi 82 kwenye hospitali na dhidi ya wahudumu wa afya na zaidi ya asilimia 90 ya mashambulizi haya yamefanyika Kaskazini Magharibi ikiwemo jimboni Idlib.”

Ameongeza kuwa hali ya hewa ya msimu wa baridi kali ikiwemo vimbunga vya karibuni, mvua kubwa na baridi kali vimesababisha hali katika maeneo hayo kuwa mbaya zaidi kwa watoto na familia zao hususan kwa wale wanaokimbia mapigano au wanaoishi makambini.

UNICEF inatoa msaada kuwanusuru

UNICEF ipo nchini Syria na inafanya kila iwezalo kuwalinda na kunusuru maisha ya watoto wakati huu wa machafuko, ghasia na baridi kali licha ya vikwazo vya kupata fursa ya kutoa msaada wa kibinadamu.

Imeongeza pia kwa kushirikiana na wadau wengine UNICEF inawafikia maelfu ya watoto kwa msaada wa mablanketi na nguo za baridi, maji safi ya kunywa, huduma za kudhibiti maji taka, huduma za afya, elimu, na msaada wa kisaikolojia ili kuwasaidia watoto kukabiliana na kiwewe cha vita walichokumbana nacho.

Hata hivyo Bi. Fore amesema “Wakati juhudi zote hizi za kuokoa maisha zikizendelea, hazitoshelezi. Kukomesha vita tu ndiko kutakakowaletea usalama wanaoutaka na kustahili watoto wa Syria. Hadi wakati huo haki zao za kuwa na amani sasa na matumaini ya mustakbali wao hayatatimizwa.”

Ombi maalum

Wakimbizi kutoka Syria wanaishia kambi ya Domiz nchini Iraq
Photo: Jodi Hilton/IRIN
Wakimbizi kutoka Syria wanaishia kambi ya Domiz nchini Iraq

 

Na mwaka huu ukianza mkuu huyo wa UNICEF amesema wanatoa ombi kwa niaba ya mamilioni ya watoto wa Syria. Tunatoa wito kwa wale wanaopigana hususan katika eneo la Kaskazini Magharibi na wale walio na ushawishi juu yao kufanya yafuatayo. Kukomesha mashambulizo yote dhidi ya watoto na huduma ambazo zinatolewa kwa watoto ikiwemo za afya, vituo vya elimu na mifumo ya maji.

Kuafikiana usitishaji uhasama mara moja Kaskazini Magharibi mwa Syria ili kutoa kipaumbele cha kuwalinda watoto, kufufua juhudi za kufikia makubaliano ya amani na kumaliza kabisa vita Syria.

Kurejea azimio la Baraza la Usalama ambalo linawezesha ufikiaji wa kibinadamu ulio endelevu na kufikiwa kwa watoto wote wanaohitaji msaada kaskazini magharibi na mahali pengine nchini Syria kupitia njia zote zinazowezekana ikiwa ni pamoja na katika mipaka ya udhibiti ndani ya Syria au mipakani mwake.

Na Bi.  Fore amehitimisha wito huo kwa kusema "Ni tumaini langu la moyoni kwamba mwaka 2020 hatimaye  utakuwa mwaka wa amani kwa watoto wa Syria."