Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wajane waanzisha kikundi cha kuwasaidia wenzao walioathirika na mapigano nchini CAR

Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
Yaye Nabo Sène/OCHA
Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Wanawake wajane waanzisha kikundi cha kuwasaidia wenzao walioathirika na mapigano nchini CAR

Wanawake

Pamoja na kukabiliwa na ubaguzi na unyanyasaji wa kingono, wanawake nchini Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR, wamechukua hatua ya kuwapatia matumaini wenzao wanaorejea katika makazi yao walimofurushwa kutoka na mapigano katika jamii zao. 

Eneo la Begoua, nje kidogoya mji mkuu wa CAR, Bangui, ni kikao cha wanawake...

Ni katika jamii ambayo wanawake wanakabiliana na kubaguliwa, katika vita ambako unyanyasaji wa kingono umetapakaa, kikundi hiki Femme Debout, cha wajane na yatima wa vita, kinachukua hatua ya kuwasajili wanawake wakristo na waislamu, kuwafundisha ustadi mpya za kuwafanya wazalishaji wa kipato kwa familia zilizoachwa bila msaada, na kuwapa matumaini kwa kuwaleta pamoja ili kwa pamoja kuponya majeraha ya madhila waliyokumbana nayo.

Florence Atanguere, ambaye naye aliwahi kuishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini CAR, ni rais wa kikundi hicho cha Femme Debout, anasema,“Mwanamke ana moyo. Mwanamke ana sauti. Mwanamke ana nguvu. Ndiyo maana tulisema: “Wanawake simama!”

Bi. Atanguere, anasema anashangaa vita ilikuwa inahusu nini kwani kabla ya hapo, wakristo na waislamu waliishi pamoja, walikuwa ndugu na hata walioana. 

Anasema alianzisha kikundi hiki kuwasaidia wanawake na wasichana kurejea na kusimama kwa miguu yao tena. Na anaongeza,“kikundi hiki kimewasaidia wanawake wengi. Tunasimama pamoja. Bila kujali ni waislamu au wakristo, bila kujali sisi ni akina nani, sisi ni wa damu moja.”

Madina yeye alimpoteza mpenziwe katika vita, na anasema,“alikuwa mkono wangu wa kuume. Hakuna anayeweza kusaidia kuyaondoa maumivu hayo. Kikundi hiki kiliokoa maisha yangu. Kabla, nilijihisi asiye na msaada,nilikuwa na mengi ya kuyashinda. Kikundi kiliniokoa.”

Kikundi cha Femme Debout kina wanawake wanachama wapatao 175, wanaotoka kote nchini. Wengi wao ni wajane wakiwa wamewapoteza waume wao kutokana na sababu za kiafya, ajali za barabarani au migogoro ya silaha.