Waliokuwa na hofu nasi, sasa wajivunie uwezo wetu- Madereva wanawake

9 Machi 2021

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifawa kuweka utulivu, MINUSCA unajivunia wanawake madereva ambao wamechukua jukumu la kusafirisha watendaji wake katika maeneo mbalimbali na hivyo kuondokana na fikra potofu ya kwamba kazi hiyo ni ya wanaume pekee. Assumpta Massoi ameandaa taarifa inayofafanua zaidi.

 

Katikati ya mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Bangui, basi la Umoja wa Mataifa likiwa limebeba wafanyakazi na kwenye usukani ni Mouno Koisset Olivia.

Yeye ni miongoni mwa madereva 7 walioajiriwa na MINUSCA na wanafanya kazi kwa zamu. Jukumu lao huanza asubuhi kwa kila mmoja kupangiwa kazi yake. Mazima Yasseko Yolande ni mmoja wao na anaeleza kwa nini aliamua kuwa dereva akisema, "wakati nilikuwa bado nyumbani, niliwaza ni kazi gani naweza kuifanya vizuri. Kufanya kazi kwanza lazima uipende na pia isaidie kile kinachokuzunguka. Kwa hiyo nikajiambia, kwa nini nisifanya udereva kuwa ni kazi. Ndipo nikaanza kazi hiyo na nashukuru Mungu nilipata msimamizi mwanamke aliyenishawishi nifanye usaili. Aliniambia alifurahi kwamba sasa kwenye idara yao watakuwa na mwanamke kwa sababu wakati huo walikuwa na wanaume pekee."

Wanawake hao wanaendesha mabasi ya kusafirisha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kutoka kazini hadi nyumbani. Mouno anazungumzia changamoto akisema,"Kuna vikwazo vingi, mathalani hapa Bangui [BO-NGI] hakuna alama za kutosha za kusimama. Naweza kusema hata bodaboda haziheshimu alama za kusimama, kwa hiyo kama hauko makini unaweza kupata ajali nyingi."

Wanawake hawa madereva wanasema watu wengi wanadhani udereva ni kazi ya wanaume tu na ndio maana hapo kuna hoja ya jinsia ambapo dereva mwingine

Feizoure Komboy anasema, "Watu ambao awali walikuwa na hofu kuhusu uwezo wetu, ni wakati wa kujivunia sasa, kwa sababu hatukukata tamaa na pia tuna mwanamke ambaye ni msimamizi wetu. Yeye anatusaidia kila wakati, na kutuhamasisha tusikate tamaa. Wale waliokuwa na hofu sasa ni wakati wa kujivunia sisi kwa sababu hatukukata tamaa."

Kwa dereva Doyemet Christelle, jambo kuu ni wto kwa wanawake akisema, "natumia fursa hii kuwaeleza kuwa msifuate kile watu wanasema. Tambueni kuwa wanawake na wanaume ni sawa, na kile ambacho mwanaume anafanya mwanamke anaweza. Awali ilkuwa udereva ni wanaume tu, lakini sasa hata wanawake wanaendesha magari, kwa hiyo njooni nanyi mfanye kazi kama yangu."

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter