Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka mfungwa hadi mkufunzi gerezani: Asante MINUSCA

Ushonaji kwa kutumia mashine
© IOM 2021/Lauriane Wolfe
Ushonaji kwa kutumia mashine

Kutoka mfungwa hadi mkufunzi gerezani: Asante MINUSCA

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR stadi za kazi zilizotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MINUSCA kwa wafungwa wanawake na wanaume, yamekuwa msaada mkubwa baada ya wafungwa hao kumaliza mafunzo na hivyo kufanikish lengo la mafunzo la ujumuishaji vema wa wafungwa katika jamii.

Kutana na Judith Ngouvela, mwenye umri wa miaka 22 na mama wa watoto wawili., mmoja umri wa miaka minne mwingine umri wa miaka miwili. 

Alitumikia kifungo katika gereza la wanawake la Bimbo kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui, ambako alikuwa miongoni mwa wanufaika wa stadi za ufumaji wa sweta. 

Kabla ya kufungwa, alikuwa anaishi jimbo la Omblella M’poko akijihusisha na biashara ya mkaa ili kutunza familia yake. 

Sasa amerejea gerezani si kama mfungwa, bali mkufunzi kwa wafungwa wengine akipatiwa na kipato. 

Judith anasema, “ninachofanya hapa nawafundisha wafungwa ufumaji wa sweta za watoto. Nilikuwa mfungwa,  sasa niko huru. Ni gerezani ambako nimepata ujuzi huu. Watendaji wa MINUSCA walifurahishwa sana na kazi yangu na wameniita nije niwafundishe wafungwa wa hapa Bimbo. Ninafundisha kwa miezi mitatu na nitapata kipato cha kutunza familia yangu.” 

Mafunzo anayotoa Judith ni kwa kutumia mashine, lakini nyumbani ingawa hana mashine mahususi, anaendeleza ujuzi wake kwa kutumia kulabu au sindano maalum ya kufumia sweta ili kufuma mitindo ya kisasa ya nguo za sweta. 

Hata hivyo anasema, “nina ujumbe kwa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanaweza kunisaidia. Kwa sababu hivi sasa kile ninachotaka kuwa nacho ili kufanikisha ndoto yangu ni kuwa na mashine maalum ya kufumia sweta, ili nijipatie kipato, pia nifundishe wengine ujuzi huu, nao wawe huru kiuchumi na pia kwa maendeleo ya nchi yetu.”