Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 30 ya haki za mtoto kuna mafanikio lakini changamoto ni kubwa kwa masikini:UNICEF 

Mjini Abidjan nchini Côte d'Ivoire, watoto wakisherehekea siku ya watoto duniani.
© UNICEF/Frank Dejongh
Mjini Abidjan nchini Côte d'Ivoire, watoto wakisherehekea siku ya watoto duniani.

Miaka 30 ya haki za mtoto kuna mafanikio lakini changamoto ni kubwa kwa masikini:UNICEF 

Haki za binadamu

Katika kuelekea siku ya kimataifa ya haki za mtoto hapo Novemba 20, ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF inasema kuna mafanikio ya kihistoria yaliyopatikana kwa miaka 30 lakini bado kuna changamoto kwa watoto masikini duniani

Ripoti hiy iliyotolewa leo iitwayo “Mkataba wa Haki za mtoto uko njia panda” inasema kwa ujumla duniani kote kumepigwa hatua kubwa kwa watoto tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za Watoto CRC miaka 30 iliyopita lakini watoto kutoka nchi masikini bado hawajayashuhudia mafanikio hayo na hivyo ripoti inatoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kufufua ahadi kwa ajili ya haki za mtoto zinazohitajika kushughulikia umri na vitisho vinavyojitokeza.

Ripoti hiyo inaangalia mafanikio yasiyopingika kwamba kuliko na utashi wa kisiasa na dhamira maisha ya watoto yameboreka.  Akizungumzia hilo mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na sasa watoto wengi kuishi kwa muda mrefu zaidi, maisha bora na yenye afya na idadi ya watoto wenye umri wa kwenda shule ambao hawahudhurii shule imepungua kutoka asilimia 18 hadi asilimia 8, muongozo wa mkataba wa haki za mtoto CRC umechagiza katiba mbalimbali, sheria, sera na kubadili mwenendo kote duniani lakini ripoti inaonyesha kwamba hatua zilizopigwa haziwiani.

“Katika nchi za kipato cha chini na cha wastan katika familia masikini kabisa kuna uwezekano mara mbili zaidi wa watoto kufa  kwa sababu zinazozuilika kabla ya kutimiza umri miaka mitano ya maisha yao ukilinganisha na familia za nchi Tajiri”

Amesema takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba ni nusu tu ya watoto kutoka familia masikini Afrika Kusini mwa Jangawa la Sahara wanapatiwa chanjo ya Surua ikilinganishwa na asilimia 85 ya watoto kutoka familia tajiri.

Vitu kama ubaguzi, umasikini na kutengwa vinaendelea kuwaacha mamilioini ya watoto wenye hali dunia katika hatari. Vita, kuongezeka kwa chuki dhidi ya wageni, uhamiaji wa kimataifa na mgogoro wa wakimbizi vyote vina athari mbaya kwa hatua za kimataifa dhidi ya haki za mtoto. Pia watoto wako katika hatari za kisaikolojia , kimwili na kimazingira kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Bi. Fore amesisitiza kwamba mkataba uko katika njia panda baina ya miongo iliyopita na uwezekano wa hatma yake, na ni jukumu letu kurejelea ahadi, kuchukua hatua na kujiwajibisha. Amesema tufuate mfano wa vijana ambao wanapaza sauti na kupigania haki zao kuliko wakati mwingine wowote, lazima tuchukue hatua sasa, hatua madhubuti na bunifu na kwamba "Haki za mtoto hazina muda wa mwisho. Tunapotarajia miaka 30 ijayo ya hatua kwa ajili ya watoto, hebu tuongeze juhudi zetu mara mbili, na ahadi zetu kuhakikisha kwamba haki hizo hazimuachi mtoto nyuma. Hebu tusongeshe ahadi ya mkataba kuhusu haki za mtoto”