Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandamano kila kona yakumbusha sauti za watoto zapaswa kusikika-UNICEF

Waandamanaji katika mitaa ya Santiago nchini Chile.
UN News/Diana Leal
Waandamanaji katika mitaa ya Santiago nchini Chile.

Maandamano kila kona yakumbusha sauti za watoto zapaswa kusikika-UNICEF

Haki za binadamu

Maandamano yanayoshuhudiwa hivi sasa katika kila kona ya dunia ni kumbusho kwamba sauti za watoto na barubaru zinapaswa kusikika na haki zao kulindwa amesema mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Bi. Henrietta Fore amesema “watoto na vijana kote duniani wamejitosa barabarani katika miezi ya hivi karibuni kudai haki zao. Ingawa kila tukio ni la kipekee, kuanzia Mashariki ya Kati hadi Amerika ya Kusini, mpakani Caribbea na Ulaya, Afrika na Asia vijana wanatoa wito wa kuchukuliwa hatua dhidi ya mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, kukomesha ufisadi na kuziba pengo la usawa, kuwepo na elimu bora, fursa ya ajira na kuwa na dunia yenye usawa kwa kila mmoja kila mahali.”

Mkuu huyo wa UNICEF ameongeza kuwa kwa hivyo ni jambo la kuumiza na kusikitisha kwamba katika kusimama kudai haki zao za msingi watoto wengi na barubaru wanapokonywa haki zao kila wakati, “mengi ya maandamano haya yamewaacha waandamanaji vijana wakiswekwa rumande, kujeruhiwa na wakati mwingine kuuawa. Shule zimesambaratishwa na huduma za umma kuingiliwa.”

Bi. Fore amesisitiza kuwa haki za watoto za kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza, ikiwemo wa kuanadamana kwa amani vimewekwa bayana katika mkataba wa haki za mtoto , mkataba ambao umeridhiwa zaidi duniani kuliko mikataba yote ihusuyo haki za binadamu. Hivyo amesema “ni jukumu la nchi wanachama kuhakikisha kwamba Watoto wanaweza kufurahia haki hizo kwa usalama na kwa njia ya amani.”

Amewataka wadau wote kujizuia na machafuko na kuhakikisha ulinzi wa msingi kwa Watoto kila mahali, wakati wote ikiwemo ambako kuna machafuko au vita vya silaha.

Amesisitiza kuwa “ombi langu ni tafadhali tuwalinde Watoto dhidi ya machafuko na kuheshimu haki zao za kuongea na kusikilizwa. Wapeni fursa za kutoa madukuduku yao na kushiriki katika masuala ambayo yanawahusu na kuathiri Maisha yao. Wasikilizeni na chukueni hatua zinazostahili, za kujenga na kuwaunga mkono.”