WHO yatoa mwongozo wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza mijini

Mwanamume wa miaka 46 aliyekatwa mguu kutokana na kisukari, moja ya magonjwa yasiyoambukiza.
Photo: IRIN
Mwanamume wa miaka 46 aliyekatwa mguu kutokana na kisukari, moja ya magonjwa yasiyoambukiza.

WHO yatoa mwongozo wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza mijini

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limetoa mwongozo na mbinu za kuwezesha viongozi kwenye maeneo ya majiji kuweza kukabiliana na visababishi vikuu vya vifo kwenye maeneo hayo.

Mwongozo huo umo kwenye ripoti iliyozinduliwa hii leo ambayo ni siku ya miji duniani, ikilenga kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kiharusi, saratani na kisukari ambayo husababisha vifo vya watu milioni  41 kila mwaka duniani kote, sambamba na ajali za barabarani zinazoua watu million 1.3 kila mwaka.

Ripoti hiyo ikitokana na utafiti uliofadhiliwa na taasisi ya Bloomberg inataja maeneo muhimu ya kupatiwa msisitizo ikiwemo kudhibiti matumizi ya tumbaku, uchafuzi wa hewa, milo isiyo na lishe, kufanya mazoezi na kuboresha usalama barabarani.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanon Ghebreyesus amesema, “zaidi ya nusu ya watu duniani wanaishi mijini, na idadi yao inaongezeka. Viongozi wa miji wanapaswa kuchukua maamuzi ambayo yataboresha afya za wakazi wao. Na ili miji iweze kuchipua na kustawi, kila mtu anapaswa kupata huduma ambazo zitaboresha afya; huduma za usafiri wa umma ziwe salama, makazi ya nje yawe safi na salama, mlo uwezo mzuri na huduma za afya ziwe bora.”

Kwa upande wake, balozi wa WHO katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs na majeraha, Michael Bloomberg amesema kwa kusambaza mikakati hiyo bora zaidi duniani kote, “tunaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.”

Bwana Bloomberg ambaye amewahi kuwa Meya wa jiji la New York kwa awamu tatu amesema, “tunafanya kazi kuhamasisha uelewa miongoni mwa viongozi wa miji na watunga sera kuhusu manufaa halisi yanayoweza kupatikana pindi programu hii ya kuboresha miji inapofanya kazi.”

Ripoti inatolea mfano mikakati inayofanya kazi kama vile hatua za kudhibiti matumizi ya tumbaku huko Beijng hadi Bogor hadi harakati za usalama barabarani huko Accra hadi Bangkok, na matumizi ya pamoja ya baiskeli huko Fortaleza bila kusahau harakati za kuweka maeneo ya watembao kwa miguu hususan wazee ambayo yamepunguza vifo vya kwa asilimia 16 jijini New York.

Ripoti hiyo inatokana na tafiti katika maeneo 19, ambapo 15 ni kutoka nchi zinazoendelea, ikionesha kuwa asilimia 85 ya vifo vya mapema vya watu wazima hutokana na NCDs na zaidi ya asilimia 90 ya vifo kutokana na ajali za barabarani viliripotiwa.

Mataifa 193 yameazimia kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ili kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030.