Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dkt. Tedros aonyesha picha halisi ya NCDs duniani, wajumbe waonyesha simanzi

Nchini Colombia mwanamke mmoja akipatiwa chanjo dhidi ya saratani ya kizazi.
PAHO.WHO.Jane Dempster
Nchini Colombia mwanamke mmoja akipatiwa chanjo dhidi ya saratani ya kizazi.

Dkt. Tedros aonyesha picha halisi ya NCDs duniani, wajumbe waonyesha simanzi

Afya

Simanzi ilionekana leo kwenye nyuso za washirki wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza baada ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus kuomba washiriki wasimame pindi tu wanaposikia ametaja ugonjwa ambao umekuwa chanzo cha kifo cha iwe ndugu, jamaa, jirani au rafiki.

Dkt. Tedros alitoa rai hiyo leo Alhamisi  kwenye mkutano wa ngazi ya  juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliokutana kujadili jinsi ya kuchagiza harakati za kuondokana na magonjwa hayo ambayo ni pamoja na kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya  njia ya hewa, saratani na msongo wa mawazo.

“Tafadhali naomba nikitaja ugonjwa na ukiona kuwa unafahamu mtu ambaye amefariki dunia kutokana na ugonjwa huu usimame,” amesema Dkt. Tedros na kisha akasoma magonjwa hayo huku akitazama hadhira kwenye ukumbi huo.

Magonjwa aliyotaja ni magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani, kisukari, magonjwa sugu ya mapafu, msongo wa mawazo, kujiua na aina yoyote ile ya shida za afya ya akili, akisema “iwe ni wewe au mtu yeyote unayemfahamu. Sioni mtu yeyote aliyeketi. Hakuna hata mmoja. Hebu fikiria ni chumba hiki tu zidisha mara elfu 82, ni sawa na watu milioni 41 wanafariki dunia mapema kutokana na NCDs.”

Mhudumu wa afya akipima kiwango cha sukari cha mgonjwa kwa kutumia kifaa maalum cha kupimia sukari mwilini.
PAHO/WHO
Mhudumu wa afya akipima kiwango cha sukari cha mgonjwa kwa kutumia kifaa maalum cha kupimia sukari mwilini.

Kadri alivyokuwa akitaja magonjwa ndivyo kadri watu walivyoendelea kusimama akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed na ndipo Dkt. Tedros akasema “hicho ndicho kiwango cha changamoto tunayokabiliana nayo, tunasimama kwa ajili ya kumbukumbu yao, tunasimama kwa mshikamano na hao ambao wasingalifariki dunia iwapo tungalichukua hatua. Tumeazimia kwa ajili ya dunia yenye afya, salama na usawa. Asanteni sana!”

Mapema mkutano huo wa tatu wa ngazi ya juu kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza ulipitisha azimio la kisiasa lenye lengo la kuchagiza harakati za kuondokana na magonjwa hayo.

Dkt. Tedros akawapongeza wajumbe kwa kupitisha azimio hilo lakini akataja mambo muhimu matatu ili kuweza kufanikisha. Mambo hayo ni utashi wa kisiasa akisema popote penye utashi wa kisiasa hakuna lisilowezekana. Jambo la pili ni uwekezaji wa ndani kwenye mifumo ya afya akisema kutumia fedha kuboresha mifumo hiyo ni faida na si hasara. Jambo la tatu ametaja kuwa ni kuimarisha huduma ya afya kwa wote akisema iwapo kila mtu atapata huduma ya afya pindi anapoitaka hata kiwango cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kitapungua.