Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 65,000 wapata chanjo Syria na msaada mwingine licha ya machafuko yanayoendelea:UNICEF/WHO/WFP

Mtoto akipatiwa chanjo ya polio kwa njia ya matone katika kituo cha afya mjini Damascus, Syria
UNICEF/Halabi
Mtoto akipatiwa chanjo ya polio kwa njia ya matone katika kituo cha afya mjini Damascus, Syria

Watoto 65,000 wapata chanjo Syria na msaada mwingine licha ya machafuko yanayoendelea:UNICEF/WHO/WFP

Afya

Kampeni ya chanjo ya polio iliyokuwa imepangwa hata kabla ya machafuko kushika kasi Kaskazini Mashariki mwa Syria imeendelea bila tukio lolote baya. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, takriban watoto 65,000 wamepatiwa chanjo hiyo katika jimbo la Hassakeh wakiwemo 1,748 kambini  Al Hol na 740 katika kambi ya Areesheh siku ya Jumatano na Alhamisi wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa UNICEF Marixie Mercado amesema kituo cha kusukuma maji cha Hassakeh bado hakifanyi kazi kutokana na uharibifu uliofanywa kwenye mtambo mkubwa wa maji, na hivyo kuathiri usambazaji wa maji kwa zaidi ya watu 400,000. Ameongeza kuwa “Fursa pia inahitajika ili kuruhusu UNICEF kuweza kufikisha lita 16,000 za mafuta kila siku kuendesha jenereta za kusukuma maji. Katika siku sita zilizopita ni asilimi 30 tu ya mahitaji ya maji nio yaliyoweza kupatikana kupitia mfumo wa maji.”

Bi. Mercado amesema UNICEF inaendelea kupeleka maji kwa malori kwenye kambi za Al Hol na Areesheh, kwenye jamii na kwenye makazi yaliyoathirika na uhaba wa maji kwenye miji ya Hassakeh na Tal Tamer.

Hivi sasa kwa mujibu wa UNICEF kazi inaendelea kukarabati vituo vya usafi, kukujenga vyoo, kuondoa maji taka na kukusanya takataka katika kambi hizo.

Pia msaada wa kisaikolojia na elimu kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini inatolewa katika, mazingira rafiki kwa watoto katika miji ya Hassakeh na Raqqa na UNICEF imeanza kugawa vifurushi vilivyo na nguo za majira ya barodi. “Tunafanya kazi kwa karibu na washirika wetu ili kubaini na kuwasaidia watoto ambao wametenganishwa na familia zao .Na timu zetu za waaguzi wanaotembea kila mahali wanafanya uchunguzi wa magonjwa makubwa yaliyoripotiwa kama kuhara na matatizo ya mfumo wa hewa.”

Timu hizo za wauhudumu wa pia zinaendesha tathimini ya lishe na kutoa mgao ikiwemo wa biskuti zenye kutia nguvu na vitu vingine vya kuongeza lishe.

Msaada kutoka mashirika mengine

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema licha ya changomoto zinazoendelea bado linaendelea kutoa msaada na huduma za msingi za afya kwa maelfu ya watu katika maeneo ambako wahudumu wa shirika hilo wanaweza kufika.

Shirika hilo limeongeza kuwa “wafanyakazi wetu wanasalia Kaskazini Mashariki mwa Syria , hata hivyo kuna haja ya haraka ya kuongeza huduma ili kukidhi mahitaji ya msingi na vifaavya muhimu vinavyohitajika  kwa ajili ya watu waliotawanywa na machafuko.”

Tani 40 za vifaa tiba na dawa vimesafirishwa kwa ndege kutoka Damascus kwenda Al Oamishly kati ya 15th na 15 Oktoba 2019. Vifaa ambavyo vitatosheleza kutoa matibabu zaidi ya 102,000 na kushughulikia visa vya wagonjwa mahtuti 620 vitagawiwa katika hospital na vituo vya afya vinavyosaidiwa na WHO katika maeneo ya Al-Hassakeh, vijiji vya Ar-Raqqa na Deir-ez-Zor.

Kwa upande wake shirika la mpango wa chakula duniani WFP linaendelea kuongeza hatua za msaada ili kuwasaidia watu 580,000 kwa mwezi huu wa Oktoba, na hadi sasa wameshawafikia watu 170,00 na msaada wa chakula tangu 9 Oktoba.

Nalo shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema wakimbizi wapya wameendelea kuwasili Iraq wiki hii iliyoghubikwa na machafuko Kaskazini Mashariki mwa Syria.

Kwa siku nne mfululizo UNHCR imekuwa ikipokea mamia ya wakimbizi wanaovuka mpaka na kuingia Iraq kutoka Syria. Na kwa mujibu wa shirika hilo wakimbizi hao wanatoka Kaskazini Mashariki mwa Syria katika miji ya Kobani, Amoda, Oamishly na katika vijiji vya jirani na maeneo hayo.