Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya siku sita misafara ya misaada yakamilika Rukban Syria:UNICEF

Misaada ya mavazi kutoka UNICEF
UNICEF/ Delil Souleiman
Misaada ya mavazi kutoka UNICEF

Baada ya siku sita misafara ya misaada yakamilika Rukban Syria:UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, washirika wa Umoja wa Mataifa na chama cha msalaba mwekundu nchini Syria, wamekamilisha misafara ya siku sita ya misaada ya kibinadamu kwenye kambi ya Rukban iliyoko Kusini Mashariki mwa Syria karibu na mpaka wa Jordan.

Huu ulikuwa ni msafara wa kwanza kuondoka ndani ya Syria kwenda kambini hapo ambako kunaishi watu takribani 50,000 wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Msaada wa mwisho kuwasili katika kambi hiyo ulikuwa mwezi Januari ukitokea Jordan.

UNICEF ilipeleka malori  21 yaliyosheheni misaada ya kibinadamu kama sehemu ya msafara na kusaidia msaada wa chanjo kwa watoa chanjo 21, kwa vifaa vya huduma za afya, vifaa vya kuhifadhia chanjo na chanjo zenyewe ili waweze kutoa chanjo kwa watoto 10,000 dhidi ya surau, polio na magonjwa mengine ya watoto kambini hapo.

Shirika hilo limeongeza kuwa hii ilikuwa moja ya operesheni ngumu za kibinadamu nchini Syria ambapo malori 75, wahudumu wa kibinadamu zaidi ya 100 na wataalamu wa kiufundi walifikisha msaada kwa watu waliouhitaji katika mazingira magumu ya jangwa Kusini mashariki mwa Syria. Mwakilishi wa UNECEF nchini Syria Fran Equiza, amesema “Watoto na wanawake kambini Rukban hawakuwa na fursa ya kupata huduma za afya hali ilizidi kuwa mbaya. UNICEF ilishirikiana kwa kila hali na washirika husika ili kujumuisha watoa chanjo katika msafara kuweza kuwalinda watoto na maradhi yanayotishia maisha yao.”

Kwa mujibu wa UNICEF watoto wengi wa chini ya umri wa miaka mitano hawakuwahi kupata chanjo yoyote kambini hapo , na licha ya changamoto zilizopo “tumefanikiwa kuwachanja watoto 5100 katika siku chache tulizopata fursa kambini hapo lakini bado tunahitaji fursa endelevu kwani maelfu ya watoto bado wanahitaji kuchanjwa” amesema afisa wa chanjo na lishe wa UNICEF aliyekuwa katika msafara huo.

UNICEF imeelezea hali kambini Rukban kuwa ni mbaya  huku watu wengi wakiishi kwa mlo mmoja tu kwa siku.

UNICEF imetoa wito kwa pande zote hasimu katika mzozo wa Syria kuruhusu wakimbizi wa ndani kurejea katika nyumba zao au katika maeneo wanatakayochagua kwa usalama na kiutu , na pia kuhakikisha fursa endelevu ya kutoa misaada ya kibinadamu kwa watoto wote wanaohitaji huduma Rukban na kwingineko Syria.