Atlasi ya saratani yazinduliwa: Rambaza ufahamu hali halisi na hatua zinazochukuliwa

16 Oktoba 2019

Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa saratani, IARC na wadau wake wamezindua toleo la tatu la atlasi au kitabu cha ramani kinachoonesha hali ya saratani duniani.

IARC ambayo ni taasisi tanzu ya shirika la afya ulimwenguni , WHO, imezindua kitabu hicho chenye ramani na michoro kandoni mwa mkutano wa kimataifa wa viongozi walio kwenye harakati dhidi ya saratani huko Astana, Kazakhstan.

Kikiwa kimepatiwa jina, Upataji huduma huchochea maendeleo, kitabu  hicho cha ramani ya hali ya saratani duniani kinampatia msomaji hali ya saratani kwa kila nchi, sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana na ugonjwa huo hatari.

Msomaji anaweza kupakua ramani, taarifa na ujumbe kuhusu vichochezi vya ugonjwa huo katika kila eneo la dunia na hatua ambazo taifa fulani imechukua kukabili.

Walengwa, kwa mujibu wa IARC ni serikali, mashirika ya afya ya umma, watunga sera pamoja na wagonjwa na manusura wa saratani na umma mzima kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa IARC, Dkt. Elisabete Weiderpass akizungumzia ramani hiyo ya ugonjwa wa saratani duniani amesema, “atlasi hii ya saratani inampatia mtu si tu uwezo wa kutambua msingi wa mzigo wa saratani na vichochezi vyake duniani, bali pia hatua za kukabiliana na ugonjwa huo kuanzia hatua kuu zinazohitaji ushirikiano wa dhati baina ya mifumo ya afya na ugonjwa wenyewe. Ni chapisho kubwa lenye vielelezo tosha vya picha vinavyokupatia tathmini na kuelezea simulizi ya manufaa ya kujizuia na saratani na kuzuia tofauti za maeneo yenye ugonjwa huo, kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo endelevu.”

Mradi wa IAEA wa kusaidia tiba dhidi  ya saratani katika nchi za kipato cha chini na kati umesaidia mataifa kutekeleza mipango mahsusi ya kutibu saratani
IAEA
Mradi wa IAEA wa kusaidia tiba dhidi ya saratani katika nchi za kipato cha chini na kati umesaidia mataifa kutekeleza mipango mahsusi ya kutibu saratani

Vigezo hatarishi

Sehemu ya kwanza ya atlasi hiyo inaangazia vichochezi tofauti vya kuenea kwa saratani katika maeneo mbalimbali duniani, vichochezi hivyo ikiwa ni pamoja na matumizi ya tumbaku, maambukizi, utipwatipwa na kupata mionzi hatari ya ultraviolet. Halikadhalika inaonyesha nini kinaweza kufanyika ili kupunguza vichochezi hivyo. Mathalani, matumizi ya tumbaku yamesalia chanzo kikuu cha saratani katika nchi zinazoendelea, lakini watu bilioni 1.5 duniani kote wanalindwa dhidi ya saratani kutokana na sera za kuzuia uvutaji tumbaku maeneo ya umma.

Mzigo wa Saratani

Sehemu ya pili ya chapisho inaangazia ramani yenyewe  ya saratani duniani kwa ukanda na kiwango cha maendeleo ya binadamu. Mathalani ulinganifu wa kunusurika saratani, wasifu wa manusura wa saratani na suala la ongezeko la gharama za matibabu. Athari za ukosefu wa usawa zinapatiwa msisitizo na suala zima la athari za saratani kwa watu wa jamii za asili na changamoto zao kwenye tiba linapatiwa msisitizo.

Kuchukua hatua

Je ni hatua zipi zimechukuliwa? Jibu linapatikana sehemu ya tatu, kuanzia kinga dhidi ya saratani hadi matibabu na huduma kwa wale waliotaabani. Akizungumzia hatua hizi, Dkt. Freddie Bray ambaye anasimamia kitengo cha saratani IARC, amesema, “chapisho hili litakuwa mbinu thabiti ya  kukabiliana na saratani.”

Aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa IAEA Yukiya Amano akikutana na mgonjwa wa saratani katika taasisi ya uchunguzi na tiba ya  saratani ya Ocean Road (ORCI)Tanzania
IAEA/Conleth Brady
Aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa IAEA Yukiya Amano akikutana na mgonjwa wa saratani katika taasisi ya uchunguzi na tiba ya saratani ya Ocean Road (ORCI)Tanzania

Hali ya Saratani Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda

Kwa kuangazia vigezo vya vichochezi, mzigo wa saratani na hatua zinazochukuliwa, altasi hiyo inakupatia uwezo wa kulinganisha nchi nchi ambapo kwa vichochezi, baina ya Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda, uvutaji sigara miongoni mwa wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea umeshika kasi zaidi Kenya kwa asilimia 20.2 ukifuatiwa na Tanzania kwa asilimia 19.9 Hata hivyo suala la utipwatipwa miongoni mwa wanawake kama kichochezi cha saratani limeshika kasi zaidi Tanzania kwa asilimia 25.8 ikifuatiwa na Kenya kwa asilimia 25.5

Kwa upande wa mzigo wa saratani, tezi dume inaongoza kwa wanaume katika nchi zote nne ilhali kwa wanawake ni saratani ya kizazi.

Je ni  hatua zipi zinatumiwa na nchi zote kukabili saratani ? Mataifa yote manne yametia saini mkataba wa kimataiwa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku, FCTC, lakini bado kuna changamoto ya kuwepo kwa lebo dhahiri kwenye pakiti za sigara kuonya watu juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku.

Hata hivyo nchi zote nne ziko mstari wa mbele kupatia chanjo wananchi wake dhidi ya homa ya ini aina ya Hepatitis B, ambapo Rwanda inaongoza kwa asilimia 98, ikifuatiwa na Tanzania asilimia 92, Kenya asilimia 78 na Uganda asilimia 78.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter