Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya kuweko kwa mbinu za kudhibiti, bado saratani yaendelea kuwa mzigo wa afya duniani

Maonesho ya bidhaa za kupambana na saratani kwenye kongamano la kwanza la taifa la saratani nchini Kenya.
UN News Nairobi/Thelma Mwadzaya
Maonesho ya bidhaa za kupambana na saratani kwenye kongamano la kwanza la taifa la saratani nchini Kenya.

Licha ya kuweko kwa mbinu za kudhibiti, bado saratani yaendelea kuwa mzigo wa afya duniani

Afya

Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa ugonjwa wa saratani umeendelea kuwa mzigo kubwa wa afya duniani na kusababisha vifo licha ya kuweko kwa mbinu za ugunduzi na matibabu, huku saratani  ya mapafu ikishika nafasi ya kwanza na ile ya titi ikishika nafasi ya pili na wadau wakitaka utashi wa kisiasa ili kutokomeza ugonjwa huo.

Taarifa iliyotolewa leo Geneva, USwisi na Lyon, Ufaransa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO inasema kauli hiyo inafuatia makadirio mapya ya mzigo wa ugonjwa wa saratani duniani, kulekea siku ya ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo tarehe 4 mwezi huu wa Februari.

Makadirio hayo yaliyotolewa na shirika la kimataifa la utafiti wa saratani, IARC ambalo ni shirika tanzu la WHO yalitokana na utafiti katika nchi 185 yakionesha kuwa idadi kubwa ya nchi zilizoshiriki hazitengi fedha za kutosha na huduma ya uangalizi wa wagonjwa wa saratani si sehemu ya Mpango wa Afya kwa Wote, au UHC.

Takwimu za maambukizi mapya, vifo na tofauti kijinsia

Mwaka 2022, kulikuweko na wagonjwa wapya milioni 20 wa saratani na kati yao hao milioni 9.7 walifariki dunia. Watu waliosalia hai miaka mitano baada ya kubainika kuwa na saratani ni milioni 53.5. 

Takwimu zinaaainisha zaidi kwamba mtu 1 kati ya 5 anapata saratani maishani, sawa na mwanaume 1 kati ya 9, na mwanamke 1 kati ya 12 anakufa kwa saratani.

WHO kupitia takwimu zake za Huduma ya Afya kwa Wote, inasema miongoni mwa nchi 115 zilizohusika na utafiti huu, ni asilimia 39 pekee (39%) ndio zinajumuisha matibabu ya saratani kwenye bima ya afya. Asilimia 28 (28%) zimejumuisha huduma ya ziada ya  usaidizi kwa wagonjwa ikiwemo udhibiti wa maumivu ikiwemo  yale yasiyohusiana na saratani. 

Saratani 3 zilizoongoza kati ya 10 mwaka 2022

Utafiti umebaini kuwa aina 10 za saratani  kati ya aina 36 ndio zilibeba theluthi mbili ya maambukizi mapya ya saratani na vifo duniani kwa mwaka 2022 katika nchi 157 kati ya 185 zilizoshiriki kwenye utafiti.

Saratani ya mapafu ikitajwa kuwa inapata zaidi wanaume,ilishika nafasi ya kwanza ikiwa na wagonjwa wapya milioni 2.5,  ikifuatiwa na saratani ya titi inayopata wanawake na nafasi ya tatu ni saratani ya utumbo mpana. Saratani ya tezi dume ilikuwa ya nne, ile ya tumbo ya tano. 

Utafiti huo unasema kuendelea kushika kasi kwa saratani ya mapafu “kunatokana na kuendelea kwa matumizi ya kupindukia ya uvutaji wa tumbaku barani Asia.”

Kipimo cha mara kwa mara cha saratani ya titi kinaweza kuepusha kushamiri kwa ugonjwa huo.
© Unsplash/National Cancer Institute
Kipimo cha mara kwa mara cha saratani ya titi kinaweza kuepusha kushamiri kwa ugonjwa huo.

Takwimu hizo zimeonesha kuwa saratani ya shingo  ya kizazi ilishika nafasi ya nane kwa kuwa na wagonjwa wapya, huku ikiwa ni ya tisa katika kusababisha vifo vitokanavyo na saratani ikiwa imekuwa na wagonjwa wapya 661,044 na vifo 348, 186.

“Ni saratani inayopata sana wanawake kwenye nchi 25, nyingi zao zikiwa nchi za AFrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Taarifa hiyo inasema pamoja na kutambua viwango mbali mbali vya ugonjwa huo, saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutokomezwa kama tatizo la afya ya umma kupitia Mpango wa WHO wa kutokomeza Saratani ya Shingo ya Kizazi.

IARC inasema vifo vingi vya saratani miongoni mwa wanaume vilitokana na saratani ya mapafu ilihali kwa wanawake ni wa saratani ya titi.

Shirika hilo linasema makadirio yake, kwa kuzingatia vyanzo bora vya takwimu vilivyopatikana mwaka 2022, yanaangazia ongezeko la mzigo wa ugonjwa wa saratani duniani, na madhara yake kwa jamii zisizopata huduma, na hivyo udharura wa kuondoa ukosefu wa uwiano wa huduma ya saratani duniani.

Tofauti kwa nchi za kipato cha juu na cha chini

Kwa nchi zenye kipato cha juu, ni mwanamke 1 kati ya 71 atakufa kwa saratani ya titi wakati katika nchi za kipato cha chini mwanamke 1 kati ya 48 atafariki dunia.

Dkt. Isabelle Soerjomataram, Naibu Mkuu wa Tawi la Ufuatiliaji wa saratani IARC anasema “wanawake katika nchi za kipato cha chini ana nafasi ya chini ya asilimia 50 kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya titi kuliko wanawake kwenye nchi za kipato cha juu, lakini wako katika hatari kubwa ya kufa kwa ugonjwa huo kwa sababu ya uchunguzi kuchelewa kufanyika na vile vile kukosa huduma bora.”

Kwa Dkt. Bente Mikkelsen, Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, WHO anasema shirika hilo linafanya kazi na zaidi ya serikali 75 kuandaa, kufadhili na kutekeleza sera za kufanikisha huduma ya saratani kwa watu wote. “Kupanua wigo wa kazi hii, uwekezaji mkubwa unahitajika haraka ili kutatua tatizo la ukosefu wa uwiano wa tiba dhidi ya saratani duniani.”

Wagonjwa wapya wa saratani 2050 kufikia zaidi ya milioni 35 duniani kote

Yakadiriwa kuwa iwapo  hatua thabiti hazitachukuliwa, mzigo wa ugonjwa wa saratani duniani utakuwa mkubwa ifikapo mwaka 2050 ambapo yakadiriwa kutakuwa na wagonjwa wapya zaidi ya milioni 35, ikiwa ni ongezeko kwa asilimia 77 kutoka makadirio ya wagonjwa milioni 20 mwaka 2022.

Ongezeko hilo la makadirio ya wagonjwa wapya linaashiria ongezeko pia la idadi ya watu duniani wakiwemo wazee, watu kuwa kwenye mazingira ya vigezo ya maambukizi kama vile matumizi ya tumbaku, maendeleo ya kiuchumi na kijamii, unywani pombe na uchafuzi wa mazingira.

Dkt. Cary Adams Mkuu wa Chama cha kimataifa cha kudhibiti saratani, UICC anasema “licha ya maendeleo yaliyopatikana kwenye utambuzi wa mapema wa saratani pamoja na tiba na huduma kwa wagonjwa, bado kuna tofauti kubwa tiba sio tu kati ya nchi za kipato cha chini na cha kati, bali pia ndani ya nchi. “Mahali mtu anaishi, hakupaswi kuamua iwapo ataishi au la pindi atakapobainika kuwa na saratani. Mbinu zipo kuwezesha serikali kupatia kipaumbele saratani na kuhakikisha kila mtu anafikia huduma. Hili si suala la rasilimali bali suala la utashi wa kisiasa.”