Kila sekunde 40, kuna mtu anajiua-WHO

10 Oktoba 2019

Mtu mmoja hufariki dunia katika kila sekunde 40 kwa kujiua, limesema shirika la afya duniani hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya afya ya akili.

Siku hii ambayo huadhimishwa Oktoba 10 kila mwaka hutumika kukuza uelewa kuhusu afya ya akili na ujumbe wa mwaka huu ni kuzuia kujiua.

Takwimu za WHO zinaonesha kuwa kila sekunde 40, mtu mmoja mahali fulani duniani anafanya maamuzi ya kujiua uhai na watu takribani 800,000 wanajiua kila mwaka na hivyo kufanya matukio ya kujiua kuwa sababu ya pili katika sababu za vifo vya vijana wadogo wa umri wa miaka 15 na 29.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  kupitia ujumbe wake kwa siku hii ya afya ya akili anasema, “afya ya akili imepuuzwa kwa muda mrefu lakini  lakini inatuhusu sisi wote na hatua zaidi inahitajika haraka.”

 

Katibu Mkuu Guterres anataka ongezeko la uwekezaji katika huduma na anaongeza, “hatutakiwi kuruhusu unyanyapaa kuwazuia watu kuomba msaada wanaouhitaji.”

Kwa mujibu wa WHO kila kisa kimoja cha kujiua, kuna visa 20 vya majaribio ya kutaka kujiua na mara nyingi hurudiwa hadi kufanikiwa. Asilimia 80 ya visa vya kujiua hutokea katika nchi za chi za kipato cha chini na kati kutokana na ukosefu wa rasilimali za kutoa msaada na kumsaidia mtu  ambaye ameathirika na msongo.

Katika siku hii, WHO inasisitiza kuwa kujiua kunaweza kuzuilika kwa kuunganisha jitihada na kuhusisha kila mtu katika jukumu hili.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter