Ajabu dunia ya leo zaidi ya watu milioni 800 hawana chakula- Guterres

Wanafamilia nchini Burkina Faso wakila mlo wao pekee wa siku (Aprili 2018)
WFP/Simon Pierre Diouf
Wanafamilia nchini Burkina Faso wakila mlo wao pekee wa siku (Aprili 2018)

Ajabu dunia ya leo zaidi ya watu milioni 800 hawana chakula- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya chakula duniani wito ukiwa ni kutokomeza njaa- na kuwa na dunia ambako chakula chenye lishe bora kinapatikana kwa bei nafuu na kwa watu wote na kila mahali, Umoja wa Mataifa unahoji iweje leo hii zaidi ya watu milioni 820 hawana chakula cha kutosheleza mahitaji yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii anasema kuwa haikubaliki kwamba njaa inaongezeka wakati ambako dunia inatupa takriban tani bilioni moja ya chakula kila mwaka.

Kama hiyo  haitoshi, amesema watu bilioni mbili, wanaume, wanawake na watoto wana uzito kupita kiasi au ni matipwatipwa na kwamba, “milo isiyo bora inazua hatari ya magonjwa na vifo.”

Katibu Mkuu amesema, “Ni wakati wa kubadilisha namna ambavyo tunazalisha, tunatumia, ikiwemo kupunguza gesi chafuzi.Kubadilisha mifumo ya chakula ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.”

Ni kwa mantiki hiyo, Bwana GUterres amesema “ndio sababu ninatarajia kuandaa kongamano la mifumo ya chakula mwaka 2021 kama sehemu ya muongo wa hatua kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.Kama familia ya binadamu, dunia isiyo na njaa ni wajibu wetu.”

Wadau wakutana Roma kujadili mwelekeo wa kutokomeza njaa duniani

Kutoka Roma, nchini Italia ambako ndiko makao makuu ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, hii leo kumefanyika tukio maalum la kuadhimisha siku ya chakula duniani.

Wazungumzaji wamejikita kwenye mada kuwa lishe bora kwa ajili ya kutokomeza njaa duniani katika mazingira ambamo kwayo mabilioni ya watu ni matipwatipwa ilihali wengine wana njaa kupindukia.

Amina Hassan/UNSocialMedia
Iweje watu milioni 820 hawana chakula?

Akifungua tukio hilo, Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte amesema, “hatua za pamoja ndio njia pekee ya kushughulikia changamoto kuu za dunia ikiwemo njaa.”

Waziri Mkuu huyo wa Italia ametoa hakikisho la nchi yake kuendelea kuunga mkono dira kilimo jumuishi kinachounga mkono hoja ya utambuzi wa kitamaduni na kusisitiza kuwa, umuhimu kutambua kuwa maendeleo ni ushirikiano wa dhati wa kimataifa kama ilivyo utashi wa kisiasa kwa lengo la kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu, ameonya kuwa njaa na utapiamlo vitakuwa vikwazo vikuu vya kufanikisha SDGs ifikapo mwaka 2030 iwapo hatua sahihi hazitachukuliwa hivi sasa.

Kwa mantiki hiyo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kila mtu, kuanzia serikali, kampuni za chakula, sekta ya umma, taasisi za utafiti na walaji ili kufanikisha watu kupata milo yenye afya na hivyo kubadili mwelekeo wa sasa wa ongezeko la njaa, utipwatipwa na unene wa kupindukia.

“Tunataka utashi wa kisiasa na ahadi za dhati. Tunahitaji kuwekeza kwenye lishe na kwa ajili ya lishe. Tunahitaji kwenda sambamba na kujenga mifumo yenye afya na endelevu,” amesema Bwana Qu.

Naye Rais wa shirika la kimataifa la maendeleo ya kilimo, IFAD Gilbert F. Houngbo amesema, “tunaweza kufikia ahadi yetu ya kutokomeza njaa. Mafanikio yetu yanategemea jinsi tunavyobadili mifumo yetu ya chakula duniani ili iweze kuwa jumuishi, ikishirikisha wanawake, vijana na watu wa jamii za asili.”

Amesema hatua hiyo itasaidia mifumo hiyo ya chakula iwe endelevu, jumuishi na inayolinda mazingira.

“Tukiwa na sera sahihi na uwekezaji sahihi kwenye kilimo na maendeleo vijijini tunaweza kuwa na dunia yenye chakula cha kutosha na kupunguza njaa na umaskini.”