Majadiliano kati ya WHO na Tanzania kuhusu Ebola yanaendelea-WHO

1 Oktoba 2019

Shirika la afya duniani WHO hii leo limesema mazungumzo ya ngazi ya juu kabisa yanaendelea kati yake na serikali ya Tanzania kuhusu tetesi zilizokuwa zinadai uwepo wa mlipuko wa Ebola nchini humo.

Tamko hilo la WHO limetolewa wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo ambapo WHO ilikuwa pamoja na mambo mengine ikieleza kuanza kwa chanjo ya Kipindupindu nchini Sudan.

Akijibu swali la kama kuna taarifa yoyote mpya kutoka kwa mamlaka za Tanzania kuhusu  fununu za uwezekano wa uwepo wa ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania, msemaji wa WHO mjini Geneva, Uswisi, Tarik Jasarevic amesema  hakuna taarifa mpya kwa sasa lakini majadiliano  yanaendelea katika ngazi za juu za mamlaka ya Tanzania na WHO,

(Sauti ya Tarik Jasarevic)

 “Kuwa wazi tu ni kwa mujibu wa uhusiano wa masuala ya kiafya kimataifa. Na ushauri wa WHO kwa  nchi ambazo hazina uzoefu mkubwa wa Ebola  ni kutuma sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Kwa mfano kwa Tanzania inaweza kufanya hivyo katika mojawapo ya vituo vya uchunguzi wa Ebola nchini Uganda. Hakuna la zaidi la kusema  zaidi ya kuwa tuko tayari kutoa msaada wowote ambao Tanzania itauhitaji na mazungumzo yanaendelea.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter