Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Surua ikiua zaidi ya watu 3, 600 DRC, WHO na wadau waendesha kampeni ya chanjo

Chanjo ya kupambana na mlipuko wa surua inafanyika katika kambi hii ya wakimbizi wa ndani ya Bunia nchini Congo DRC, (Julai 2019)
© UNICEF/Marixie Mercado
Chanjo ya kupambana na mlipuko wa surua inafanyika katika kambi hii ya wakimbizi wa ndani ya Bunia nchini Congo DRC, (Julai 2019)

Surua ikiua zaidi ya watu 3, 600 DRC, WHO na wadau waendesha kampeni ya chanjo

Afya

Shirika  la afya ulimwenguni, WHO na wadau wamezindua kampeni ya dharura  nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko mkubwa wa surua ambao  hadi sasa umesababisha vifo vya watu zaidi ya 3,600.

 

Katika kijiji cha Masi Manimba, jimbo la Kwilu, nchini DRC, video ya WHO inawaonyesha watoto wakichezea puto , punde wageni wanafika, ni hali ya mgeni njoo mwenyeji apone kwani wageni hawa  ni wahudumu wa afya kutoka WHO

Mmoja wao ni Helene Chenge ambaye anasema, “surua ni ugonjwa mbaya sana. Unaua na unaweza kuwa na madhara makubwa.”

Nats...

Kisha tangazo kwa wanakijiji kuja pamoja. Huku janga la Surua linalokua kwa kasi kubwa likiendelea kushuhudiwa nchini DRC, serikali, WHO na wadau wameanzisha kampeni ya tatu ya tatu ya dharura mwaka huu ya utoaji chanjo dhidi ya surua katika vituo 24 wakilenga watoto 825,000 wenye umri wa kuanzia miezi 6 hadi miaka mitano.

Kampeni hii itafikisha idadi ya waliochanjwa hadi milioni 4.1 katika kanda za kiafya 121 kati ya kanda 192 zilizoathirika. Mhudumu wa afya ya umma Chenge tena..

(Sauti ya Helene Chenge)

“Kuna sababu nyingi kwa nini watoto hawachanjwi, wakati mwingine wazazi wanaacha kuleta watoto kwenye kliniki lakini wakati mwingine chanjo hazipatikani.”

Kando na kampeni zinazoungwa mkono na WHO, wadau wengine wamefanya kazi na serikali kuandaa kampeni za chanjo kufikia leo Oktoba Mosi. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasambaza chanjo na kuzihifadhi katika maeneo salama katika vituo sita jimbo la Oriental.Bi Chenge anasema,

(Sauti ya Helene Chenge)

“Sisi wote watoa huduma wa afya tunahitaji kukumbusha wazazi kupeleka watoto wapate chanjo wakati wowote. Tunahitaji pia kuhakikisha kwamba chanjo hzio zinapatikana.”

WHO imezindua kamati ya kukabiliana na surua kwa ajili ya kuchagiza juhudi dhidi ya mlipuko.

Kufikia tarehe 17  ya mwezi uliopita wa Septemba, wagonjwa shukiwa 183,837 wa surua walikuwa wameripotiwa huku kati yao, 5, 989 wakithibitishwa kuugua surua katika kanda 192 kati ya 519 nchini kote .

Halikadhalika watu 3667 wamekufa kutokana na Surua ikiwa ni idadi kubwa ya vifo ikilinganishwa na vifo kutokana na ebola huku waathirika karibu wote wakiwa ni watoto.