Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini wazindua kampeni ya nchi nzima kuwalinda watoto milioni 2.5 dhidi ya surua

Picha ya maktaba ikionesha WHO na wadau wengine walipopeleka msaada wa kudhibiti ugonjwa wa surua katika eneo la West Darful mwezi April 2015 nchini Sudan. Huduma kama hiyo sasa iko katika majimbo ya Sudan Kusini
WHO Sudan
Picha ya maktaba ikionesha WHO na wadau wengine walipopeleka msaada wa kudhibiti ugonjwa wa surua katika eneo la West Darful mwezi April 2015 nchini Sudan. Huduma kama hiyo sasa iko katika majimbo ya Sudan Kusini

Sudan Kusini wazindua kampeni ya nchi nzima kuwalinda watoto milioni 2.5 dhidi ya surua

Afya

Ikiwa na lengo la kuwafikia watoto milioni 2.5 dhidi ya Surua, kampeni ya chanjo nchi nzima imeanza hii leo nchini Sudan Kusini.

Kampeni hiyo ni ushirikiano kati ya Wizara ya afya ya Sudan Kusini, Muungano wa chanjo ulimwenguni, Gavi, shirika la afya duniani WHO, UNICEF na wadau wengine. Zaidi ya chanjo, pia watoto wanapewa virutubishio vya Vitamini A na vidonge vya kudhibiti minyoo.

Ripoti ya WHO na UNICEF imeeleza kuwa kampeni hiyo ni muhimu kwa afya ya watoto nchini Sudan Kusini, wakati huu ambao nchi bado inapamnana na mlipuko mbaya wa surua ambapo tayari visa 4700 vilithibitishwa na vifo 26 tangu mwezi Januari mwaka jana 2019 hadi kufikia sasa.

“Tunahitaji kuongeza chanjo ili kuwalinda watoto dhidi ya milipuko wa surua” ameeleza Dkt Makur Matur Kariom wa Wizara ya Afya ya Sudan Kusini akiongeza kusema, “Kwa bahati mbaya, katika Sudan Kusini chanjo ya mara kwa mara dhidi ya surua inabakia katika kiwango cha chini cha asilimia 59 pekee. Kwa maana hiyo watoto wengi katika nchi yetu hawalindwi dhidi ya ugonjwa.”

Kampeni hiyo itaendeshwa kati awamu mbili ambapo awamu ya kwanza imeanza leo na itaenda kwa takribani asilimia 70 ya kaunti zote katika eneo lililokuwa Equatoria ya kati, Equatoria ya mashariki, Jonglei, Lakes, Bahr el Ghazal kaskazini, Bahr el Ghazal Magharibi, Warrap na Upper Nile. Awamu ya pili itaenda katika kaunti zilizobaki za Equatoria ya kati, Jonglei, Unity, Upper Nile na itahitimishwa tarehe 17 mwezi Machi mwaka 2020.

Taarifa hiyo ya WHO na UNICEF imesema chanjo hii si tu inawalenga watoto ambao hawajachanjwa, bali pia wale ambao walishapata chanjo moja ya awali wanakaribishwa.

“Kila mtoto ana haki sawa na hakuna mtoto aliyeko mbali sana.” Ameeleza Dkt Mohamed Ag Ayoya, mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Kusini.