Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akizuru visiwa vya Bahama Guterres ataka hatua zaidi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Hali halisi ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga Dorian katika bandari ya Marsh, kisiwa cha Abaco katika visiwa vya Bahama (11 Septemba 2019)
UN Photo/Mark Garten)
Hali halisi ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga Dorian katika bandari ya Marsh, kisiwa cha Abaco katika visiwa vya Bahama (11 Septemba 2019)

Akizuru visiwa vya Bahama Guterres ataka hatua zaidi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Viongozi wa dunia watakaohudhuria mkutano unaokuja wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi  kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa wametakiwa kuja wamejizatiti sio na hotuba bali mipango ya kufikia malengo ya kupunguza hewa ukaa na kuimarisha mnepo dhidi ya changamoto hiyo ya kimataifa. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza hilo Ijumaa wakati wa ziara yake katika visiwa vya Bahama ambavyo vinaendelea kukabilianana athari ya kimbunga Dorian. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yako katika maeneo yaliyoathirika zaidi ya Abaco na makao  makuu ya Bahama ili kutoa msaada muhimu unaohitajika . 

Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu  Nassau, Katibu Mkuu ameelezea mshikamano wa kimataifa na serikali na  watu wa visiwa vya Bahama. “Katika baadhi ya maeneo zaidi ya robo tatu ya majengo yamesambaratishwa, hospitali zimehatibiwa au kuzidiwa vibaya, shule zimegeukavifusi. Maelfu ya watu wataendelea kuhitaji msaada wa chakula, maji na malazi na wengine wengi  wanahabiliwa na hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wao baada ya kupoteza kila kitu.”   

Bwana Guterres amesema anatambua kwamba mabadiliko ya tabianchi yamesababisha zahma kubwa, vikiwemo vimbunga vinavyotokea mara kwa mara vikiwa na athari kubwa. Na amesema bila hatua za haraka, uharibifu wa mabadiliko ya tabianchi utakuwa  mbaya zaidi katika kile alichokiita zahma mara tatu.   
“Mosi athari mbaya zaidi zinazikumba nchi ambazo uchafuzi wake wa gesi ya viwandani ni mdogo, visiwa vya Bahama ni moja ya mifano mzuri wa hali hiyo. Pili ni watu wasikini kabisa na wasiojiweza katika nchi hiyo ndio wanaokuwa wahanga wakubwa na kwa mara nyingine hilo pia imetokea katika jamii za visiwa vya Bahama na tatu vimbunga vinavyojirudia huzikwamisha nchi katika mzunguko wa majanga na madeni.”   
Wakati gharama za kimbunga Dorian bado hazijafahamika Bwana Guterres amekadiria kwamba itakuwa katika matrilioni ya dola.  “Visiwa vya Bahama haviwezi kutegemewa kubeba gharama hizo peke yake. Majanga haya makubwa ya mabadiliko ya tabianchi yanahitaji hatua za pamoja. Ufadhili dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni moja ya vipengee hivyo . Ni lazima tufikie lengo la dola bilioni 100 kwa mwaka kutoka kwa vyanzo vya sekta za umma na binafsi, ili kuweza kukabili na kujenga mnepo katika nchi zinazoendelea kama zilivyoahidi nchi tajiri kwa karibu muongo mmoja uliopita. Tunapaswa kuboresha fursa ya ufadhili wa maendeleo. Katika hali kama ya visiwa vya Bahama naunga mkono kwa nguvu zote mapendekezo ya kubadili madeni kuwa uwekezaji wa kujenga mnepo.”   


Mbali ya yote Guterres ametoa wito wa hatua zaidi kimataifa

Katibu Mkuu amesema “Jumuiya yote ya kimataifa ni lazima kushughulikia mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi kupitia malengo na hatua za utekelezaji wa mkataba wa Paris.Ushahidi mzuri wa kisayansi kama ulivyowasilisha na jopo la kimataifa  kuhusu mabadiliko ya tabianchi unasema ni lazima uhakikishe kwa pamoja kwamba kiwango cha joto duniani hakipindukii nyuzi joto 1.5 . Na kwamba tuna miaka chini ya 11 ya kubadili hali ya kuwa na janga la hali ya hewa lisiloweza kubadilika na  kwamba tunapaswa kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 na kufikiakiwango cha kupunguza  hewa ukaa ifikapo 2050. Na hii ndio sababu kwa nini nawaomba viongozi wote kuja kwenye mkutano wa hatua dhidi ya  mabadiliko ya tabianchi mjini New York siku chache zijazo wakiwa na mipango”   

Ziara kwenye makazi ya waathirika waliohamishwa

 Akizuru makazi ya waathirika wa kibunga Doriani waliohamishwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekutana   na waathirika hao ambao wengi walikuwa wakimbizi kutoka Haiti na kupongeza msaada wa mshikamano uliotolewa na  serikali ya visiwa vya Bahama  na watu binafsi. Amesema uwepo wa wakimbizi wengi wasiojiweza unadhihirisha ni jinsi gani msaada wa kimataifa ulivyo muhimu, “ili kuvisaidia visiwa vya Bahama kukabiliana sio tu na athari ya kibunga hicho bali pia na mahitaji mengine ya kuweza kusidia watu wake wasiojiweza  na wageni nchini humo ambao wengi  hawana nyaraka.”   

Amerejelea wito wa umuhimu wa kuchua hatua sasa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

“Ni hali isiyokubalika kabisa kwamba  tunafadhili uchimbaji wa mafuta machafu, ni suala lisilokubalika kwamba idadi kubwa ya viwanda vya makaa ya mawe vinajengwa duniani. Ni suala lisilokubalika kabisa kwamba hatufanyi juhudi kuweka gharama kubwa kwenye hewa ukaa. Endapo hatutabadili  hali hii tutashuhudia majanga kama hili yakiongezeka na kuwa makubwa zaidi na ya mara kwa mara.”   

Alipoulizwa jukumu la Umoja wa Mataifa  katika kukabiliana na athari za kimbunga hicho Guterres amesema  kwamba kuongeza kasi ya juhudi za kimataifa ni ufunguo "Kwa sababu kuna msaada mwingi wa lazima unahitajika mara moja na kuna ujenzi mpya ambao pia utahitaji mshikamano.  Na wakati huohuo sote tunahitaji kufanya kila liwezekanalo kupunguza hatari ambazo zimekuwa na athari kubwa katika visiwa vya Bahama na njia za kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa ufanisi zaidi.”