Watano wamethibitika kufariki kutokana na kimbunga Dorian-OCHA

Muonekano wa kimbunga Dorian juu ya visiwa vya Bahama
windy.com
Muonekano wa kimbunga Dorian juu ya visiwa vya Bahama

Watano wamethibitika kufariki kutokana na kimbunga Dorian-OCHA

Tabianchi na mazingira

Kimbunga Dorian kikiendelea kuleta madhara huko visiwa vya Bahamas, ripoti zinasema kwamba watu watano wamethibitishwa kufariki dunia huku mashirika ya Umoja wa Mataif ana wadau wakiwa wamepeleka watendaji wake kufanya tathmini ya uharibifu. 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada ya kibinadamu OCHA, imesema kuwa kasi ya upepo wa kimbunga doriani ni maili 157 kwa saa na kimeyapiga maeneo ya Elbow Cay katika visiwa vya Abaco vyenye wakazi 17,200 na kimeendelea kubaki juu ya kisiwa cha Grand Bahama, kaskazini mwa mkusanyiko wa visiwa vya Bahama ambako kunakadiriwa kuwa na wakazi 51,000.

Jens Laerke amewaeleza wanahabari kuwa kuna vifo vilivyokwisha thibitika,

(Sauti ya Jens Laerke)

“Waziri mkuu wa visiwa vya Bahama amesema kuwa watu watano wamethibitika kufariki dunia kutokana na kimbunga Dorian.”

Nayo Mamlaka inayoshughulikia dharura katika visiwa vya Bahamas NEMA, inakadiria kuwa watu 76,000 wako katika hatari ya kukumbana na upepo huo mkali wenye kufanya uharibifu kati yao takribani asilimia 22 ni watoto chini ya umri wa miaka 15, huku zaidi ya asilimia 70 wakiwa ni watu wa umri kati ya miaka 15 hadi 64.

Bwana Laerke ameeleza kuwa madhara yanayotegemewa yanaonesha kuwa maji yatakuwa kipaumbele,

(Sauti ya Jens Laerke)

“Mahitaji ya kipaumbele katika tathmini yetu ya awali ni kurejesha mifumo ya maji lakini pia chakula, mifumo ya kujisafi, makazi na pia matibabu.”

Wakati huo huo WFP imesema imetuma wataalamu wake wanne ambao watasaidia katika suala la uhakika wa chakula, mawasiliano ya dharura na mipango na sasa wanasubiri kibali cha serikali ili waanze kazi.