Tunasonga mbele pamoja katika kujenga amani, imani na kuaminiana-Shearer

5 Septemba 2019

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS na Tume iliyoundwa upya ya pamoja ya uangalizi na tathimini, JMEC wamefanya hafla maalum kwa lengo la kuchagiza amani na kuimarisha akataba wa amani wa mwezi  Septemba mwaka 2018.

(Play Nats)

Hafla hiyo ambayo iliwakutanisha wakazi, wawakilishi wa serikali na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu Sudan Kusini, David Shearer ambaye pia ni mkuu wa UNMISS huku kukisheheni vicheko, nyimbo na dansi kutokana na tumbuizo zilizotamalaki

Takriban wakazi 2000 kutoka maeneo jirani ya vitongoji vya mji mkuu, Juba walisikiliza na kutizama watu ambao walisimulia mitizamo yao huku baadhi ya wanawake viongozi wakisimulia madhila waliyoyapitia wakati wa mzozo. 

Mmoja wa wanawake hao ni Agnes Antorny kutoka kaunti ya Luri

(Sauti ya Agnes)

“Sisi wanawake katika eneo hili tulikuwa tumechoka, Saa moja usiku tulisikia milio ya risasi na hatukujua  sababu ni ipi na matokeo yake ni kwamba tulijificha chini ya vitanda.”

Naye Maria Gideon kutoka kundi la wanawake amesema

(Sauti ya Maria)

“Kunahitajika kuwepo na serikali mpya ambayo itaundwa kwa ajili ya watu wa Sudan Kusini ili kuwe na fursa za kazi. Sote tunahitaji kufanya kazi, tunahitaji kula, tunahitaji kuishi katika nyumba zetu kwa amani, kwa hiyo uundaji wa serikali utakuwa ni muhimu sana kwa ajili ya watu wa Sudan Kusini.

Kufikia sasa kumekuwa na nyongeza ya muda wa kutekeleza mkataba wa amani ambao kwa mujibu wa Waziri wa Habari na Mawasiliano,  mkataba utatekelezwa ndani ya muda na kufikia Novemba 12 mwaka huu ambapo serikali itakuwa imeundwa.

Mkuu wa UNMISS, David Shearer amesema utayari wa Umoja huo kusaidia kufikia amani nchini humo.

(Sauti ya Shearer)

“Tuna sitisho la mapigano kwa sasa na tunasonga mbele pamoja katika kujenga amani, imani na kuaminiana miongoni mwa pande mbali mbali.

Kwa sasa matarajio ni kwamba wenyeji na wananchi kote nchini watafurahia matunda ya amani kupitia majadiliano miongoni mwao na wengine zaidi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud