Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani yaimarika Akobo, Sudan Kusini, wananchi warejea kusongesha maisha

David Shearer, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Um,oja wa Mataifa Sudan Kusini akutana na wakazi wa Akobo
Picha ya UNMISS/Amanda Voisard
David Shearer, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Um,oja wa Mataifa Sudan Kusini akutana na wakazi wa Akobo

Amani yaimarika Akobo, Sudan Kusini, wananchi warejea kusongesha maisha

Amani na Usalama

Nchini Sudan Kusini, mkataba bora zaidi wa amani uliotiwa saini kati ya serikali na upinzani umeendelea kuzaa matunda kwa kuwa hivi sasa wananchi waliokuwa wamekimbilia nchi jirani wameanza kurejea nyumbani ili kujenga upya maisha yao. 
 

Mjini Akobo kwenye jimbo la Gilo nchini Sudan lKusini, anaonekana Nyabang Juol Chan akiandaa chai nyumbani kwake. Ghasia mjini humo zilimfurusha hadi Ethiopia lakini miezi miwili iliyopita alirejea hapa nyumbani.

Nyabang anasema “naishi hapa kwasababu nafanya kazi sokoni ili nipate fedha na watoto wangu waishi. Nauza chai wanangu wapate mchuzi, samaki au nyama. Ndio maisha yangu hapa na ni bora kuliko ilivyokuwa kambini.”

Umoja wa mataifa ulichukua hatua kuimarisha ulinzi kwenye mji huu wa Akobo kwa kuanzisha kituo kipya cha ulinzi wa amani huku wadau wa kibinadamu nao wakisindikiza wakimbizi wa ndani kutoka kambini Bor hadi Akobo.

David Shearer ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini na anasema kuwa “kile tunaona na kusikia kutoka kwa watu niliozungumza nao ni kwamba usalama hasa mapigano kati ya vikosi vya serikali na vikundi vya upinzani yamepungua. Hata hivyo kuna ongezeko la mapigano ya kikabila ikijumuisha ujangili, utekaji watoto na mauaji ya raia hili linanitia hofu na tutashughulikia kupitia kitengo chetu cha masuala ya raia ili kuepusha visasi na kupunguza matukio hayo.”

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS unaangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya walinda amani kwenye eneo hilo na kusaidia zaidi harakati za maridhiano baina ya vikundi vya kikabila ili hatimaye wananchi wajenge maisha yao na waishi kwa amani.